DAR ES SALAAM: LICHA ya kutumia nguvu nyingi kukanusha habari
zinazochapishwa na Magazeti Pendwa ya Global Publishers kuwa, amerejea
kwenye matumizi ya madawa ya kulevya ‘unga’, hatimaye staa wa Bongo
Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ amenaswa ‘laivu’ akiwa ‘ameangusha gari’
kando ya barabara, habari ndiyo hiyo!
Ray C ambaye kila
anapoandikwa na Magazeti ya Global kuhusu kurejea kwenye unga, amekuwa
akimtupia shutuma Mkurugenzi wa Global, Eric Shigongo kwamba anamchafua,
alinaswa na mapaparazi wetu hivi karibuni maeneo ya Mwananyamala
Magengeni, Dar akiwa amezima yeye na mwanaume aliyekuwa naye hali
iliyompa urahisi paparazi wetu kuwafotoa picha za kutosha.
ISHU ILIANZA JANUARI
Januari mwaka huu, gazeti hili liliripoti habari iliyokuwa na kichwa; CHIMBO LA UNGA LA RAY C LAGUNDULIKA.
Baada ya habari hiyo kutoka, Ray C aliikanusha kupitia ukurasa wake wa Instagram akisema:
“Seriously kwa kweli huwa naumia sanasana kuona binadamu mwenzangu
anadiriki kuniharibia jina langu ili yeye apate kula! Hamjui mnaniathiri
kiasi gani na hizi habari zenu! Hiyo habari yaani ni ujingaujinga tu
umeunganishwa na picha yangu bila hata uoga mmeichukua kutoka kwenye
page yangu ya Insta. Mnazitumia kunichafulia jina langu tena wakati
ndiyo kwanza nahangaika kurudi kwenye kazi yangu.”
TV ANDAGRAUNDI IKAMSAPOTI
Kama hiyo haitoshi, kituo kimoja cha runinga cha muda mrefu nchini
lakini bado kiko ‘andagraundi’ kilimpa nafasi Ray C akanushe habari ya
Ijumaa Wikienda pasipo kujua gazeti hili lilijiridhisha kabla ya
kuandika habari hiyo.
SHIGONGO ATAKA UKWELI
Baada ya Ray C
kuyaponda Magazeti ya Global kwenye runinga kwa kudai yanamchafua,
Shigongo alimuagiza Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa, Oscar Ndauka
kupanga makachero kutokea kwenye kikosi maalum cha Oparesheni Fichua
Maovu ‘OFM’ ili kufuatilia nyendo za msanii huyo kama kweli anaonewa au
la na kutaka matokeo yaliyo kamili!
OFM KAZINI
Timu ya OFM
ilipangwa kwa zamu kumfuatilia Ray C kwa saa ishirini na nne ili
kujiridhisha juu ya malalamiko yake, hasa kwamba Global inaungaunga
picha za zamani ili kupata habari kama alivyosema kwenye Instagram yake.
Tangu
Januari hiyo, timu ya OFM ilianza kuwa sambamba na Ray C huku makachero
wengine wakiwasaka watu wake wa karibu ili kusikia chochote kutoka
kwao.
MSIKIE HUYU
“Mimi ni miongoni mwa watumiaji wa madawa ya
kulevya ambaye nilishawishiwa na Ray C kuacha na kunileta hapa kwenye
Kituo cha Mwanayamala (hospitali) kwa ajili ya kuanza kumeza Methadone
(dawa za kuponya waathirika wa madawa ya kulevya) ili niweze kurudia
hali yangu ya kawaida. Hali yangu sasa niko safi na najitambua.
AMSIKITIKIA RAY C
“Kinachoniuma ni Ray C ambaye aliniunganisha hospitali kwa mbwembwe,
yeye ameshindwa kuendelea na kapata bwana ambaye amemsaidia kurudia tena
matumizi ya unga kushinda zamani. Huwezi amini kwa sasa mwenzetu gari
limewaka upya, anawasumbua hata madaktari wetu, wakati mwingine wamekuwa
wakishindwa kumhudumia.
FULL VURUGU
“Akija hapa kituoni
kuchukua dawa muda wote ni kuwasimanga hawa wauguzi wetu jambo ambalo
linatukera sana kwani anatuharibia hata sisi ambao alituleta.
Aliyemponza ni Frank. Frank alikuja hapa kituoni kama mwathirika na
kuanza kutumia dawa.
“Baada ya kukutana na Ray C na kuwa marafiki,
wameshindwa kuendelea kutumia dawa. Badala yake wamekuwa wakivuta unga
kiasi cha kuzima na kuleta fujo tu. Huyu Frank anaishi Mwananyamala
karibu na hapa hospitali,” alisema mwathirika mmoja akiomba kufichiwa
jina lake.
MADAKTARI WALIMSUSA
Akaendelea: “Unajua madaktari
wa hapa walifikia hatua ya kujivua kumhudumia na kumrejesha kwao
kipindi kile alipofanya fujo Posta. Ninasema haya kwa uchungu maana hata
sisi tunaokunywa naye dawa hakuna hata mmoja anayeweza kummudu zaidi ya
huyo Frank ambaye naye gari limeshachanganya, anampoteza kabisa Ray C,”
kilisema chanzo hicho.”
JK ANYOOSHA MIKONO, AMUACHIA MAGUFULI
Chanzo kingine kilichopo kwenye hospitali hiyo kililiambia Ijumaa
Wikienda kuwa, kutokana na JK kumsaidia alipokuwa madarakani na mrembo
huyo kurejea tena kwenye unga, amenyoosha mikono, jukumu hilo litabaki
kwa rais wa sasa, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’.
“JK
ameshanyoosha mikono. Hawezi tena kumuelewa huyu dada, amemuachia
Magufuli naye labda ajaribu kwani ndiye aliyeko madarakani,” kilisema
chanzo hicho.
RAY C MWENYEWE HUYU HAPA
Alipotafutwa Ray C juzi na kusomewa madai hayo na kuelezwa juu ya kupigwa picha zinazomuonesha akiwa amezima, alifunguka:
“Kweli
kuna picha nimesikia watu walinipiga nikiwa nimezimika lakini siyo
kwamba nilivuta unga kiasi hicho, picha hizo nilipigwa kweli nikiwa
nimezima baada ya kunywa dawa hapo hospitali maana dawa ninazokunywa
huwa ni kali sana, saa nyingine huwa nashindwa kujizuia na kujikuta
nimezima.
“Kwanza unatakiwa ujue kwamba hizi dawa siku zote
ukinywa hata kama ungekuwa na nguvu kiasi gani lazima kuna muda unafikia
hatua ya kushindwa kabisa kujimudu na saa nyingine huwa tunalala hata
na wenzangu kwani hata hizo picha wamenipiga chini ya mti hapahapa
jirani na eneo la hospitali, siku hiyo nilikuwa nimezidiwa sana.”
AMTAJA FRANK KAMA ‘BEBI’ WAKE
“Ninachokijua nilala chini ya mti na Frank lakini hata ukiangalia nyuma yetu pia
kuna
watu kibao ambao nao walikuwa wamelala baada ya kunywa dawa na
kuzidiwa, sasa sijui wewe hizo zangu na huyo mpenzi wangu umezitoa
wapi,” alisema Ray C.
DAKTARI WA WAATHIRIKA AZUNGUMZA
Baada ya
utetezi huo wa Ray C, gazeti hili lilimwendea hewani daktari wa tiba
kwa waathirika na unga kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (jina lipo)
na kumuuliza kama matumizi ya dawa za Methadone yanaweza kumzimisha
mtumiaji ambapo alisema:
“Kama anayetumia Methadone baada ya
kuathirika hatatumia madawa ya kulevya hawezi kuzima kwa namna yoyote
ile. Ukimwona mtu anazima ujue anachanganya, yaani anameza Methadone pia
anaendelea kubwia unga.”
TUMEFIKAJE HAPA?
Ray C aliyewahi
kutamba na nyimbo nyingi kali, ikiwemo Na Wewe Milele, alijikuta
ametopea kwenye madawa ya kulevya baada ya kutumbukia kwenye uhusiano wa
kimapenzi kwa staa wa Hip Hop Bongo, Isaac Waziri Makuto ‘Lord Eyez’
ambaye naye anadaiwa kutumia.
Baadaye wawili hao walimwagana huku
Ray C akichanja mbuga katika eneo hilo hali iliyomlazimisha ‘kustaafu’
muziki kutokana na mwili kukosa mawasiliano katika kupanga mikakati.
Gazeti damu moja na hili, Ijumaa, toleo Namba 799 la Novemba 2-8, 2012
lilitoa picha za Ray C akiwa amezimika na habari yenye kichwa; DAH!
RAY C. Tukio hilo lilijiri maeneo ya Magomeni, Dar.
JK ASOMA, APATA UCHUNGU
Wiki moja baada ya gazeti hilo kuingia mtaani likielezea hali ya Ray C,
JK alimwita Ikulu ya Dar es Salaam yeye, mama yake mzazi, Margaret
Mtweve na ndugu mwingine hali iliyoonesha kuwa, aliisoma habari hiyo
kwenye Gazeti la Ijumaa.
Lengo la kumwita lilikuwa kumsaidia
mwanamuziki huyo kwa tiba na uangalizi wa kina jambo ambalo lilifanyika
na akarudia kwenye hali yake ya kawaida.
Mwaka 2015, baada ya
minong’ono mingi kwamba msanii huyo amerejea katika matumizi ya unga,
magazeti ya Global yaliandika habari hiyo na Ray C akawa anakanusha mara
kwa mara mpaka majuzi aliponaswa akiwa amezima.


0 comments:
Post a Comment