Saturday, March 19, 2016

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm ameweka bayana falsafa yake ya kucheza soka la kushambulia kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya APR ya Rwanda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo.

Yanga inarudiana na APR mchezo wa raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwenye mchezo wa awali uliochezwa Kigali wiki iliyopita, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Hans-van-der-Pluijm
Kutokana na ushindi huo, Yanga ina nafasi nzuri ya kusonga mbele, kwani inahitaji sare ama ushindi wa aina yoyote kusonga leo. Lakini pamoja na kuwa kwenye hali hiyo kimchezo, Pluijm amesema hatacheza soka la kujihami kusonga mbele. “Unajua falsafa yangu kuhusu mchezo wa soka.

Tutashambulia tunapotakiwa kushambulia na kujilinda tunapotakiwa kujilinda. Tunatakiwa kuwapa kitu fulani mashabiki wetu wazuri,” alisema Pluijm. Yanga itajivunia kurejea kwa nyota wake ambao walikosekana kwenye mchezo uliopita ambao ni winga Geofrey Mwashiuya na mshambuliaji Malimi Busungu waliokuwa wagonjwa.

Mabao ya beki wa pembeni Juma Abdul na kiungo Thabani Kamusoko yanaweza yasitoshe kwenye mchezo wa leo kama APR wakifanikiwa kupata bao la mapema na hivyo Yanga hawana budi kucheza kwa tahadhari kubwa na zaidi kutafuta ushindi.

Bao moja la APR kwenye uwanja wake wa nyumbani linaweza kuwa mwiba mchungu kwa Yanga kuelekea mchezo wa leo na hivyo safu ya ulinzi ya Yanga itakayokuwa chini ya Vincent Bossou na Kelvin Yondani haina budi kucheza kwa umakini mkubwa.

Lakini pia washambuliaji Donald Ngoma, Amis Tambwe na wengineo wanapaswa kuhakikisha wanaifungia timu yao bao la mapema litakaloipa APR mtihani mkubwa wa kusawazisha na kuibuka na ushindi.

Pamoja na kuundwa na wachezaji wengi chipukizi APR bado ni timu hatari kwa Yanga na lolote linaweza kutokea. Naye Rahel Pallangyo anaripoti kuwa kocha wa APR, Nizar Kanfir, alisema mchezo wa kwanza walifungwa mabao 2-1 na sasa ni zamu yao kurudisha kipigo hicho kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

“Yanga ni timu nzuri walitufunga kwetu kwenye dakika 90 za kwanza sasa ni zamu yao nao kufungwa kwani tunahitaji kusonga mbele na siyo kukamilisha ratiba,” Kanfir.

0 comments:

Post a Comment