SERIKALI imesema kama Shirika la Afya Duniani (WHO), litapitisha
matumizi ya dawa mpya ya ugonjwa Ukimwi wataitumia, lakini kwa sasa
haiwezi kuzungumzia tafiti za ugonjwa huo ambazo zipo nyingi.
Akizungumza na MTANZANIA juzi jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael
John, alisema kwa sasa zipo tafiti nyingi, lakini wao kama wizara
wanasubiri mwongozo kutoka WHO ambao ndiyo unathibitisha ubora wa dawa
na matumizi yake.
“Zipo tafiti nyingi tunazisikia zinafanyika, lakini hili la Ukimwi ni
mapema mno kulizungumzia ila kinachohitajika ni kusubiri mwongozo wa
WHO ambao ndio wanatuongoza kwenye orodha ya dawa na matumizi yake
katika magonjwa mbalimbali,” alisema John.
Juzi mashirika mbalimbali ya habari yalitoa taarifa juu ya utafiti
mpya wa dawa ya mseto ya kimiminika ijulikanayo kama PrEP ambayo
inatarajiwa kuleta faraja kwa wenza ambao mmoja anaishi na virusi vya
Ukimwi huku mwingine akiwa hana.
Dawa hiyo inadaiwa tayari imeanza kutumika kwa baadhi ya mashoga
nchini Uingereza na Marekani ambapo huweza kuondoa hatari ya kuambukizwa
hadi asilimia sifuri. Pia itaondoa changamoto iliyokuwapo katika njia
namba moja ikiwa pamoja na kujikinga na virusi vya Ukimwi, yaani kutumia
kondomu wakati wa kufanya tendo la ndoa.
Kutokana na matumizi ya kondomu wenzi hao walikuwa hawawezi kupata
watoto bila uwezekano wa kuhatarisha afya ya mwenzi ambaye hana VVU.

0 comments:
Post a Comment