Diamond
Makala; Ojuku Abraham
DIAMOND
Platnumz atakuwa mmoja wa wasanii watatu wanaofanya muziki barani
Afrika, ambao watapanda katika jukwaa la ukumbi maarufu wa Barclays
Centre, jijini New York nchini Marekani, Julai 22, mwaka huu wenye uwezo
wa kuingiza watu 20,000 katika tamasha lililopewa jina la One Africa.
Wengine
watakaoungana naye ni Wizkid na Flavour kutoka Nigeria, ambao kwa
pamoja watakuwa wasanii wa kwanza wanaofanyia muziki barani Afrika
kuwahi kutumbuiza kwenye ukumbi huo uliozinduliwa mwaka 2012 kwa shoo
kubwa ya rapa Jay Z.
Maana
yake ni kuwa Diamond atakanyaga jukwaa ambalo mastaa kama Rihanna,
Justin Bieber, Bayonce na wengine wamefanya na hivyo kujiwekea historia
ya kuwa msanii wa kwanza Bongo kufanya hivyo, kwani mara nyingi Wabongo
wamekuwa wakifanya shoo Ulaya na Marekani katika kumbi ndogondogo na
wakati mwingine hata uani kwa mtu.
Wabunge
wawili vijana wanaoheshimika na jamii ya Bongo Fleva, Joseph Mbilinyi
(Sugu) na Joseph Haule (Profesa Jay) ambao ni wakali wa Hip Hop wa muda
wote Tanzania, wamekiri kuwa ilikuwa ni kilio chao siku zote, kutaka
wasanii wafikie hatua iliyofikiwa na Diamond.
“Ninaufahamu
huo ukumbi ni mkubwa sana kwa kweli, kumuona mtu kama Diamond anakwenda
kufanya shoo pale ni jambo la kufurahisha sana. Kwa maoni yangu, muziki
wa Bongo unakwenda kubatizwa rasmi pale, kwamba sasa tunaingia katika
ramani halisi ya dunia kimuziki,” anasema Profesa Jay.
Alisema
anafurahishwa sana na jitihada binafsi zinazofanywa na Diamond kiasi
kwamba sasa amekuwa msanii mkubwa Afrika, jambo linalomtia moyo, hasa
akikumbuka siku kijana huyo kutoka Tandale alipomwaga machozi mbele
yake.
“Nilipomuuliza
analia nini, aliniambia hakuwahi kuwaza maishani mwake kama kuna siku
anaweza kufanya wimbo na Profesa Jay, hakuwahi kuamini kama anaweza
kufikia levo zangu, jambo hili lilinigusa sana na najua mimi ni mmoja wa
wasanii waliom-inspire kuupenda na kuufanya muziki,” alisema mkongwe
huyo aliyemshirikisha Diamond katika kibao chake cha Kipi Sijasikia.
Jay
alisema Diamond anawa-inspire vijana wengi kutokana na juhudi zake na
mafanikio anayoyapata ni ishara kwamba ukiwa na nia na kitu utafanikiwa
kama utajibidisha.
“Ni
jambo jema kabisa kwamba Diamond sasa anatubeba wasanii wote, lazima
tumpongeze maana anakoelekea, ndiko tulikokuwa tukipigania miaka yote.”
Kwa
upande wake, Sugu alisema siku zote alikuwa katika harakati za kutaka
msanii wa nchi hii aheshimike, hatua ambayo Diamond amefikia.
“Natambua
uwezo wake na jitihada zake, mimi sizungumzii tu muziki, bali biashara
ya muziki, tunataka tuwe na ma-CEO wasanii, watu ambao tunaweza
kutengeneza ajira kupitia muziki. Katika hotuba yangu kama Waziri Kivuli
wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, nimeitaka serikali
kutoa mwongozo kwa redio na televisheni nchini, kupiga asilimia 80 ya
muziki wa nyumbani na unaobaki ndiyo uwe wa nje.
“Maana
huwezi kufahamika kimataifa bila kwanza kufahamika nyumbani, tunataka
hivi kwa sababu tunahitaji kuwa na akina Diamond wengi, akina Samatta
(Mbwana, mwanasoka) wengi, kwa hiyo ni lazima serikali itoe fursa hizi,
siyo mtu anajibidisha mwenyewe, akipata mafanikio mtu wa serikali
anajitokeza kumpongeza kana kwamba walijihusisha naye.
“Diamond
anafanya vizuri sana na kwa kweli tunajivunia, tunataka tuwe kama
wenzetu Nigeria, kule kuna akina P Square, Davido, 2Face Idibia na
wengine wengi wanafahamika kimataifa, au DRC wapo akina Koffi Olomide,
Fally Ipupa, Feregora, Werasson na wengine na sisi tunatakiwa tuwe na
kina Diamond, Ali Kiba, AY, yaani tuwe nao wengi,” anasema Sugu.
Barclays
Center ni ukumbi unaotumika kwa shughuli mbalimbali na upo Brooklyn,
New York City. Pia hutumika kama uwanja wa nyumbani wa timu ya kikapu ya
Brooklyn Nets pamoja na New York Islanders ya National Hockey League.
0 comments:
Post a Comment