WAKATI Rais John Magufuli wa Tanzania akishikilia msimamo kuwa nchi
yake haitasaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) na Umoja wa
Ulaya (EU) mpaka dosari kadhaa zitakaporekebishwa, baadhi ya wabunge wa
EU wamemuunga mkono na kutahadharisha mkataba wa sasa utaua viwanda vya
ndani.
Siku kadhaa zilizopita, msimamo wa Tanzania na Burundi ulilazimisha
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kukubaliana kusogeza mbele
makubaliano ya ama zote zisaini mkataba huo au la ili kuruhusu uchambuzi
zaidi.
Tayari nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zimekubaliana na mkataba huo
wa EPA huku Tanzania na Burundi zikitoa sababu nzito za kiuchumi,
zinazolenga kuhakikisha kuwa kabla ya kusaini mkataba huo, ni vyema
suala la ulinzi wa viwanda vya ndani likazingatiwa.
Mkataba huo unapaswa kusainiwa na nchi zote ili uanze kutumika katika ukanda mzima.
Chini ya mkataba huo ambao majadiliano yake yalianza tangu mwaka
2007, EU inaahidi kuzipatia bidhaa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki
soko kwa kutotozwa kodi zinapopelekwa kwa nchi wanachama wa Ulaya,
lakini na yenyewe italeta bidhaa zake katika soko la ukanda bila kutozwa
kodi. Hata hivyo, msimamo wa Tanzania umesimama katika ulinzi wa
viwanda vya ndani, hasa wakati huu Serikali ikijikita zaidi katika
uchumi wa viwanda.
Msimamo huo sasa unaungwa mkono na wabunge wawili wa EU, Marie Arena
na Julie Ward, ambao wanashauri Afrika Mashariki isisaini mkataba huo wa
ubia kwa namna ulivyo sasa.
Katika mahojiano yao maalumu na mwandishi wa mtandao wa jarida
mashuhuri la The New Times, wabunge hao wanasema bayana kuwa uamuzi wa
Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki wa kuahirisha kusaini ubia huo hadi
mwakani ili watafakari zaidi uko sahihi.
“Tunaamini mkataba huu kwa namna ulivyo sasa hauko sawa. Ulaya
inaitumia Kenya ambayo ndiyo yenye maslahi zaidi katika mkataba huu kuwa
kama ngao yao. Wakati Kenya ilishaendelea kiviwanda, hali sio kama
hivyo kwa Tanzania, Uganda na Burundi ambazo hazitafaidika.
“Iwapo bidhaa za Ulaya zitaruhusiwa kuingia tu katika ukanda wa
Afrika Mashariki italeta ushindani usio wa haki na zaidi nchi hizo
zitapoteza kodi katika baadhi ya bidhaa na pia baadhi ya viwanda
vitashindwa ushindani na kufa,” wanasema wabunge hao.
Wabunge hao wananukuliwa wakisisitiza kuwa kutokana na hali hiyo,
wamejitolea kuzisaidia nchi kama Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa
kuzishinikiza nchi za Ulaya zipitie upya ubia huo na kuanzisha mfumo
mpya wenye manufaa kwa pande zote.
“Tunadhani nchi hizi zinapaswa kusubiri mpaka zote zitakapoingia
katika uchumi wa kipato cha kati ndipo zinaweza kuingia mikataba kama
hii yenye kuleta ushindani wa kibiashara. Kwa Rwanda na nchi nyingine za
EAC sisi tunaona kwa sasa wangeimarisha kwanza soko lao la ndani katika
ukanda huo,” wanaongeza wabunge hao.
Wabunge hao wanafafanua kuwa kwa sasa Kenya, ambayo imeshaingia
katika uchumi wa kipato cha kati inaweza kufaidika, lakini wanaonya nchi
nyingine hazitafaidika na EPA mpaka hapo watakapofikia uchumi wa kati.
Walipoulizwa ni kwa nini wakiwa wabunge wa Ulaya, bado wanapingana na
mkataba huo utakaoipa faida za kiuchumi jumuiya yao, wabunge hao
walijibu:
“Hoja yetu sio kupinga biashara na Afrika Mashariki, tunachotaka ni
kuona ubia huu unanufaisha pande zote. Tunazo taarifa nyingi za kitafiti
hata kutoka Kituo cha Kimataifa cha Biashara zinazoonesha kuwa mkataba
huu utakuwa na hasara kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.”
Wabunge hao wanazidi kufafanua kuwa mikataba mibovu inayoingiwa na
Ulaya na Afrika inaathari nyingi ikiwemo kusababisha umasikini Afrika na
matokeo yake kuleta athari mbaya kwa Ulaya ikiwemo kuongezeka kwa
wahamiaji haramu

0 comments:
Post a Comment