Siku ya pili ulifanyika mkutano mkubwa Mnazi Mmoja ambao gazeti la
Zuhra lilikadiria kuwa zaidi ya watu 25,000 walihudhuria. Baada ya
mapokezi na mkutano mkubwa, ukafanyika mkutano Mtaa wa Kipata na Sikukuu
nyumbani kwa Clement Mohamed Mtamila mkutano ambao ulihudhuriwa na Titi
Mohamed, Iddi Faiz Mwafongo, Tatu bint Mzee, Asha Ngoma, Mzee Haidari
Mwinyimvua na Nyerere. Katika mkutano huo Nyerere aliwaambia wajumbe
kuwa Father Walsh amemuambia ama achague siasa au aendelee kufundisha.
Mkutano ukamshauri aache kufundisha ili awe Rais wa chama"Full time" ili
kufanikisha wazo hili, Dossa Aziz alijitolea kumlipa mshahara hadi
ushindi utakapopatikana.
Ahadi hii aliitimiza. Hizi ndizo
zilikuwa harakati za Dossa Aziz. Mzee Dossa akijibu hoja iliyokuwa
ikipandikizwa kubadili historia ya kudai uhuru kuwa ati TAA kilikuwa
chama cha starehe, Dossa alisema kuwa mtafiti yeyote anaesema kuwa TAA
kilikuwa chama cha starehe na aende kwa Nyerere amuulize ikiwa mwaka
1953 alipojiiunga na chama alijiunga kwa minajili ya kujistarehesha au
kwa ajili ya siasa. Mzee Dossa alieleza kuwa suala la kupotoshwa kwa
historia ya Tanganyiika lilianza kujitokeza mara tu TANU ilipoanza
kupata nguvu na viongozi wapya kuingia katika chama hasa baada ya
Uchaguzi wa Kura Tatu mwaka 1958 na akasema kuwa hashangai kuwa leo kuna
watu wanabeza juhudi zao na kudai kuwa siasa ilikuja na Nyerere kutoka
Butiama.
Tarehe 27 Aprili, 1985 Julius Kambarage Nyerere, sasa
akijulikana kama ''Baba wa Taifa,'' katika sherehe kubwa katika viwanja
vya Ikulu, alitoa jumla ya medali 3979 kwa Watanzania waliochangia
katika maendeleo ya taifa. Kati ya wale ambao walipewa medali hizo
alikuwa Sheikh Abdallah Chaurembo. Wazalendo waliotajwa ndani ya kitabu
hiki ambao walipigania uhuru wa Tanganyika, hakuna hata mmoja wao
aliyekuwa katika orodha ile ya heshima. Baada ya siku chache kupita,
Nyerere kama mtu aliyegutuka alimualika Dossa Aziz Ikulu. Dossa Aziz,
wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika alikuwa mtu maarufu, mwenye nafasi,
na kujiweza sana. Sasa Dossa baada ya miaka kupita hakuwa akifahamika
tena na ule umaarufu na utajiri wake ulikuwa umetoweka. Alikuwa akiishi
maisha ya kawaida kijijini Mlandizi, maili chache nje ya Dar es Salaam.
Katika sherehe ya faragha Nyerere alimtunukia medali Dossa Aziz, rafiki
yake wa zamani.
Mwandishi wa makala hii alipomtembea Dossa Aziz
nyumbani kwake Aprili, 1987 ilikuwa asubuhi kiasi cha saa nne na
alimkuta Mzee Dossa amekaa barazani kwake akiwa amefungulia radio yake
akisikiliza BBC. Mara alipotambulishwa kwake alimpokea kwa ukarimu
mkubwa. Ukarimu ulikuwa ndani ya damu ya Dossa.
Mbele ya baraza
yake yalikuwepo mabaki ya Landrover ambayo Dossa alimfahamisha mwandishi
kuwa gari ile aliitumia na Nyerere katika safari za kutembelea majimbo
ya Tanganyika kwa niaba ya TANU wakati wa kudai uhuru. Mzee Dossa
akionyesha kidole mabaki ya gari yake alisema, "Gari hii imetembea
sehemu nyingi sana nikimpeleka Nyerere sehemu tofauti za Tanganyika na
katika siku za mwanzo mimi mwenyewe ndiye nilikuwa nikiiendesha gari hii
hadi pale tulipomwajiri Said Kamtawa kama dereva wa TANU." Hata kwa
wakati ule Mzee Dossa alionyesha dalili zote za kupigwa na maisha.
Katika picha ya pamoja ya waasisi wa TANU kuna watu wawili tu ambao
wanaonekana wamevaa suti na tai, hao ni Abdulwahid Sykes na Dossa Aziz.
Ishara tosha ya hadhi zao. Waliobaki wote wamejivalia mavazi yao ya
kawaida. Nyerere akiwa amevaa kaptula na soksi ndefu zilizogota
magotini, mavazi maarufu wakati ule kwa wasomi. Picha hii imebeba maneno
elfu moja. Dossa aliyeonekana pale kibarazani Mlandizi si yule
aliyekuwa kwenye picha ya waasisi wa TANU. Dossa mtanashati, mtoto wa
Mwafrika tajiri, Aziz Ali, Waziri Dossa Aziz aliyetoa mali kuipa TANU
ili Nyerere aitumie katika shughuli za kuikomboa nchi alikuwa amechoka
akionyesha dalili zote za kusahauliwa na nchi aliyoipigania ijitawale.
Dossa Aziz ni kati ya wazalendo ambao historia imedhulumu haki zao za
kutambulika kama mashujaa wa uhuru wa Tanganyika. Kwa kipindi cha zaidi
ya miaka thelathini si CCM wala si rafiki yake mpenzi Julius Nyerere
alikuwa anafahamu Dossa anaishi vipi na ana hali gani. Rafiki zake
wachache waliokuwa wakimtembelea nyumbani kwake pale Mlandizi
walihuzunishwa na hali yake. Dossa mtu aliyekuwa na mali katika miaka ya
1950 alikuwa akiishi katika hali ya ufukara. Hali hii ya ufukara
ilitaka kumkosesha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa CCM mwaka1987 pale Kizota
ambapo waasisi wote wa TANU walialikwa. Sababu kubwa ilikuwa ni ukosefu
wa nguo na viatu vya kuvaa katika hadhara kama hiyo. Ilikuwa mmoja wa
marafiki zake wa zamani Abbas Sykes ndiye aliyemnunulia nguo na viatu
vya kumwezesha kwenda Dodoma. Rafiki zake walipomshauri aende kwa
Nyerere ampatie msaada Dossa alijibu kuwa yeye hawezi kulifanya hilo kwa
kuwa Nyerere anajua kuwa yeye alitumia fedha zake nyingi katika
harakati za kudai uhuru na kama yeye Nyerere leo kamsahau yeye hana
sababu ya kumfuata. Jibu la Dossa lilikuwa jibu la muungwana, mtu
asiyekubali kujidhalilisha.
Kauli hii ya Dossa na msimamo wake
huu thabiti ulithibitishwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe siku ya Jumapili
tarehe 19 Aprili 1998 katika khitma ya marehemu nyumbani kwa Dossa pale
Mlandizi wakati Nyerere aliposimama kusema machache katika hadhara ile
kuhusu uhusiano wake na Dossa na mchango mkubwa wa marehemu Dossa Aziz
katika kuleta uhuru wa Tanganyika. Nyerere alisema kuwa hata siku moja
Dossa hakupata kumuomba kazi au kuonyesha dalili za kutaka ukubwa.
Mwalimu Nyerere aliposema maneno haya alibubujikwa na machozi na
waliokuwepo nao walilia kwa huzuni.Subira aliyokuwanayo Dossa ndiyo
sababu kubwa iliyomfanya astahamili dhiki kwa miaka yake ya mwisho ya
uhai wake na afe masikini katika hospitali ya Tumbi, Kibaha badala ya
St. Thomas Hospital, London, Dossa hakuwa wa kwanza kukutwa na haya.
Haya yalimkuta Mzee Mshume Kiyate, Sheikh Mohamed Ramia na wengine
wengi. Baada ya kuleta uhuru wazalendo hao wakageuzwa ganda la muwa.
Hakuna unachoweza kufanya na ganda la muwa ulilolifyonza ila kulitema tu
na kama utaweza kuelekeza mdomo wako kwenye jalala na kutembea humo
hivyo ni bora zaidi kwani hata kulitema ganda hilo kwenye mkono wako wa
kushoto kisha kulitupa jalalani ni kulipa hadhi ganda hilo.
Habari za Dosa Aziz zinahitaji utafiti wa kina wa msomi makini. Hii ni
changamoto kwa wana historia, wana historia wa Tanzania ya leo. Ni
katika kuijua historia ya uhuru wa nchi hii ndipo wenye madaraka hivi
sasa wanaweza kujua kwa nini hii leo wajukuu wa akina Dossa wameiona
dhulma na wanapambana na polisi na askari wa kuzuia fujo kwa mawe kisha
wanachoma moto ofisi za CCM ambacho asili yake ni mababu zao.
DOSA AZIZ NA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Ilikuwa kawaida ya Dossa baada ya mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja
kumchukua Nyerere na gari lake kumrudisha Pugu. Njia ya zamani kwenda
Pugu ilikuwa inapita hapo kilipo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa
ilikuwa kiza kimeingia na walitaka kutoka nje ya gari kuangalia mandhari
ya Dar es Salaam maana kutokea pale mji ulikuwa unapendeza sana kwa taa
zilizokuwa zikiwaka barabarani. Nyerere alimwambia Dossa, “Dossa
tukipata uhuru wetu hapa lazima tujenge chuo kikuu.” Hili wazo
lilifanyiwa kazi na wananchi wakahamasishwa kuchangia ujenzi wa Chuo
hicho. Fedha zilichangwa na Chuo kikajengwa pale New Street kwenye
kiwanja cha John Rupia alichokitoa kuwapa TANU. Hapo ndipo kilipoanza
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. (Chuo hiki sasa ni Chuo Cha Watu Wazima).
Abdallah Salum alikuwa mmoja wa wachangiaji wa chuo hicho na mwanaye
Salum Matimbwa hadi leo amehifadhi stakabadhi ya malipo ya sh. 50.00
stakabadhi ambayo ina sahihi ya Bhoke Munanka. Wazee hawa walikuwa
wazalendo wa kweli kabisa. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 na
zilipokuwa zikianzishwa harakati za ushirika Abdallah Salum Matimbwa
alitoa lori lake Commer Fargo DSY 435 kama mtaji kuingiza katika Coast
Region Transport Company (CORETCO). Pamoja naye katika kuanzisha CORETCO
walikuwa wazee wengine kama Sharia Bofu na nduguye Ibrahim Bofu, Salum
Kambi, Juma Mzee na wengineo.
***
Mtafiti na Mwanahistoria
Nguli, Mzee Mohamed Said angali hai hadi hii leo, Kwa kwenye kuhitaji
histori ya Tanganyika, anaweza kumtembelea na kuonana naye Dar es
Salaam. |
0 comments:
Post a Comment