News
MSHITAKIWA katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Salum
Njwete (34) ‘Scorpion’, amekiri kupata mafunzo ya kareti kutoka chuo cha
mafunzo cha Ifakara aliyoyafanya mwaka 1989 hadi 1995.
Aidha, upande wa mashitaka katika kesi hiyo umemuongezea mashitaka
ya shambulio kupitia kifungu namba 234 cha Sheria ya Makosa ya Jinai
ambacho kinaruhusu kuongeza au kubadilisha mashitaka.
Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga alidai jana mbele ya Hakimu
Mkazi, Flora Haule kwamba kesi hiyo imekuja kwa ajili ya mshitakiwa
kusomewa maelezo ya awali ambapo katika maelezo ya zaidi ya saa nane,
alikiri kuhusu jina lake, sehemu anayoishi ya Machimbo Yombo na mafunzo
hayo.
Hata hivyo, alikana kuhusu jina la Scorpion, mashitaka yake na kwamba hakukamatwa wala kuhojiwa na Polisi kuhusu mashitaka hayo.
Katuga alidai kuwa Septemba 6, mwaka huu, mshitakiwa alikuwa maeneo
ya Buguruni Sheli na kwamba Septemba 12, alihojiwa na kukamatwa na
polisi maelezo ambayo aliyakana.
“Mashahidi watakaotoa ushahidi katika kesi hii wapo sita ambapo
upande wetu wa mashitaka utawasilisha vielelezo viwili ikiwemo Fomu
namba tatu ya Polisi (PF3) na ripoti ya daktari kwa ajili ya
kuthibitisha mashitaka hayo,’’ alidai Katuga.
Hakimu Haule aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 14 mwaka huu,
kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kusikilizwa. Katika mashitaka yake,
mtuhumiwa inadaiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu katika
maeneo ya Buguruni Sheli, wilaya ya Ilala.
Inadaiwa, Njwete aliiba mkufu rangi ya fedha wenye uzito wa gramu
34 wenye thamani ya Sh 60,000, bangili ya mkononi na fedha taslimu Sh
331,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya Said Mrisho.
Inadaiwa kabla na baada ya wizi huo, alimchoma kisu machoni, tumboni na mabegani mlalamikaji ili ajipatie mali hizo.

0 comments:
Post a Comment