Sunday, January 1, 2017

Mmiliki na Mkurugenzi wa bendi ya muziki wa dansi ya The African Stars 'Twanga Pepeta' Asha Baraka 'The Iron Lady' amekutanishwa LIVE katika FNL ya EATV na nyota wake wawili aliowafungashia virago hivi karibuni mwimbaji Rogert Hega na rapa Ferguson



Hatua hiyo ni baada ya kuwepo kwa utata kuhusu wasanii hao kuachana na bendi hiyo na kwenda kuanzisha bendi yao inayokwenda kwa jina la Dar es Salaam Super Sound Music Band bila kumuaga bosi wao huyo.
Katika kipindi hicho kilichoruka usiku wa jana, Asha Baraka alitangaza rasmi kuachana na wasanii hao, huku wao pia wakiridhia maamuzi hayo na kuagana kwa amani hali iliyomaanisha kuvunjika kwa ndoa yao rasmi.
Akielezea sababu za maamuzi hayo, Asha Baraka alisema kuwa wasanii hao walikiuka taratibu za kinidhamu za bendi hiyo kwa kutoroka kwa kisingiio cha kuugua, na kwenda kwenye mashindano ya marapa.
Sababu nyingine ni hatua ya wanamuziki hao kuanza harakati za kuanzisha bendi nyingine ya muziki wakati bado wakiwa kwenye bendi ya Twanga Pepeta.
Ferguson
Asha amesema kuondoka kwa wanamuziki hao hakutaathiri bendi hiyo na kwamba ni hatua nzuri kuwafungulia nafasi za ajira wasanii wengine wachanga, huku akiwaasa wanamuziki hao kubadilika na kujipanga katika kazi yao na bendi yao mpya ili na wao watoe ajira kwa wengine.
Kwa upande wao, wanamuziki hao wamekanusha tuhuma zilizotolewa na Asha Baraka na kusema kuwa si kweli kwamba walikuwa na mpango wa kuanzisha bendi isipokuwa waliitwa kwenye tamasha na kisha alitokea mtu akawapiga picha na kuzisambaza zikionesha kuwa wametambulisha bendi mpya.
"Hatukutambulisha band alitokea mtu akatupiga picha, akatangaza kwenye mtandao kwamba tuna band mpya, Mama alikurupuka baada ya kusikia maneno maneno. Bendi hiyo ya DSS bado ipo kwenye mchakato baada ya kuwa vifaranga wa mama kuku aliyechinjwa" Walisema wanamuziki hao
Rogert Hega
Akifafanua hoja hiyo, Asha alisema kuwa baada ya kusikia tetesi, alitoa taarifa rasmi kuwa mtu atakayeshiriki katika bendi nyingine atakuwa amejifukuzisha kazi "Wananionea kwa kuwa sijui kuimba ningekuwa najua ningekuwa najua, nilitoa taarifa kuwa atakayekwenda kwenye tamasha kajifukuzisha kazi, kwahiyo walijua, wala sikukurupuka"
Baada ya mabishano ya takriban dakika 40, pande hizo mbili zilikubaliana kutengana rasmi huku wanamuziki hao wakitangaza rasmi kuja na bendi yao binafsi itakayoitwa Dar es Salaam Super Sound Music Band (DSS)

0 comments:

Post a Comment