Wednesday, January 4, 2017

Rapa King Crazy GK ambaye sasa anafanya vyema na wimbo wake 'Mzuri pesa' amefunguka na kuweka wazi sababu kubwa ya wasanii wa Bongo na watu maarufu nchini kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.

King Crazy GK alisema hayo alipokuwa akiongea na EATV na kutaja sababu kuu kuwa ni kutokana na wasanii hao kukosa elimu na kutumiwa kubeba unga kutokana na wao kukosa elimu.
GK alisema msanii kama Jay Z huwezi kumbebesha dawa za kulevya kwa sababu tayari ni mtu mwenye maarifa yake, mtu mwenye biashara zake na anajitambua lakini anakiri kuwa wasanii wengi na watu maarufu nchini ni wajinga ndiyo maana inakuwa rahisi wao kubebeshwa dawa za kulevya sababu watu walio na akili zao wanawatumia kama mapunda kubeba dawa za kulevya.
"Unajua sisi wasanii huwa tunaheshimika sana hata katika viwanja vya ndege huwa hatusachiwi sana hivyo wasanii wengine wanaitumia nafasi hii vibaya na kubeba madawa ya kulevya na wanafanya hivi kutokana na kukosa elimu. Leo hii huwezi kumbebesha mtu kama Jay Z dawa za kulevya sababu kwanza anajitambua lakini ni mtu mwenye mafanikio makubwa hivyo hawezi kutumika kubeba unga hata siku moja" alisisitiza King Crazy GK
Kufuatia sakata hilo King Crazy GK amewashauri wasanii na watu mbalimbali nchini kuhakikisha wanaitafuta elimu ili siku mambo yakienda vibaya kwenye muziki awe na uwezo wa kufanya mambo mengine na kuendesha maisha yake pasipo kuteteleka na kujikuta wanaingia kwenye matatizo ya dawa za kulevya.
"Wasanii wanatakiwa kuitafuta elimu sana kwani wanapaswa kutambua muziki unapanda na kushuka ukiwa na elimu yako muziki hata ukishuka unaweza kwenda kufanya mambo mengine kupitia taaluma yako na ukaendesha maisha yako vizuri, elimu kwa msanii ni kama 'Life Insurance' yake usipokuwa na elimu mambo yakiyumba ndiyo wanajikuta wanatumiwa na watu wenye akili zao kufanya mambo ya ajabu ajabu. Lakini pia wasanii wanatakiwa watambue wao ni kioo cha jamii hivyo wakiwa na elimu ni rahisi kuilisha jamii vitu vizuri kupitia nyimbo zao lakini tukiendelea kuwa na wasanii wajinga wajinga jamii itaendelea kulishwa mambo ya kijinga na kuiharibu jamii yetu" alisema King Crazy GK 

0 comments:

Post a Comment