Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es
Salaam jana, Makonda alitaja orodha ya watu 65 akiwataka kuripoti polisi
ijumaa feb 10 2017 kwa ajili ya mahojiano.
Miongoni mwa waliotwa ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,
Diwani wa Mbagala (CCM) na mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji na mbunge
wa zamani, Idd Azzan ambao walizungumza na kueleza kutofurahishwa na
hatua hiyo.
Mbowe aliyekuwa safarini kwenda bungeni Dodoma, alisema ameshangazwa kutuhumiwa kwa jambo asilolijua.
“Kama amemtaja mbunge wa Hai anajulikana ni mmoja, hata kama asingesema Freeman, Mbunge wa Hai anajulikana ni Freeman Mbowe. “The only thing (kitu pekee) ninaweza kusema nchi haiendeshwi
hivyo. Yametajwa majina mengi ambayo sijui Makonda ana evidence
(ushahidi) gani!
“Anasema tukiwaita tukiridhika na maelezo yao tutawaachia. Huwezi
kusema tu, yaani kwa kusema ni Mbowe… mimi ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, mimi ni mbunge, mimi ni mzazi, nina wanachama,
maaskofu, mapadri, mashehe na viongozi mbalimbali.
“Unapokuwa unamhusisha kiongozi na ‘drug trafficking au drug
business’ (usafirishaji wa dawa au biashara ya dawa za kulevya), sijui
ana ushahidi gani hadi akanihusisha na jambo hilo, mimi sielewi, kwa
hivyo siwezi kusema kwa kitu ambacho sielewi,” alisisitiza Mbowe.
Mbowe aliendelea kusema kuwa kesi za dawa za kulevya hazina
dhamana, hivyo alimtaka Makonda awe na ushahidi wa kutosha anapowataja
watuhumiwa.
“Tuache habari ya kuitwa, wewe umepata tuhuma, hujafanya uchunguzi,
hakuna mtu aliye juu ya sheria, lakini unatakiwa kufanya uchunguzi ili
ukimkamata mtu unamshtaki, siyo unataja mtu unachafua hadhi yake. Halafu
ukija kusema hatuna ushahidi juu yako umeshaharibu jina lake,” alisema
na kuongeza:
“Mimi sijui kama jeshi la polisi linafanya kazi hii au ni Makonda
amejipa kazi ya kuwa mpelelezi. Au labda yeye kwa kuwa ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ndiyo amejipa kazi ya kutaja majina kwenye
mambo yenye kashfa kama haya? Sielewi. This is very wrong precedence
(Hii ni rejea mbaya) kwa utawala wa sheria.”
Mbowe alisema inawezekana ni mikakati ya Serikali kuendelea kukandamiza upinzani kwa kuwakamata viongozi wake.
“Sijui kama kuna watu wanaolengwa, lakini tumeona viongozi wetu
wanakamatwa hawapewi dhamana, (Tundu) Lissu amekamatwa, (Godbless) Lema
amekamatwa … mtu anakaa miezi minne, kwa hiyo wanaweza kufanya lolote.
Inawezekana ni mkakati wa kutesa wapinzani. Wamenitafuta kwenye biashara
wameona haitoshi… sina uhakika lakini sioni kama wana nia njema na
sisi,” alisema Mbowe.
Alipoulizwa kama ataitikia wito wa Makonda, Mbowe alisema bado anawasiliana na wanasheria wake kabla ya kuchukua hatua.

0 comments:
Post a Comment