Daktari Bingwa wa Macho wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
Christine Mataka ambaye alimpokea na kumhudumia, Said Mrisho anayedaiwa
kutobolewa macho na Salum Njwete maarufu Scorpion akiwa shahidi wanne
katika kesi hiyo upande wa serikali, ametoa siri nzito ya tukio hilo.
Dokta Mataka amesema alikuwa daktari wa kawaida kwa muda mrefu
lakini alitunukiwa digrii ya pili (Master’s) na kuwa daktari bingwa wa
matatizo ya macho miaka 14 iliyopita.
Akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Nasoro Katuga bingwa
huyo alisema macho ya Said hayakutobolewa kama inavyosemwa na watu
kwenye vyombo vya habari isipokuwa yamenyofolewa na kuondolewa kabisa.
Majeruhi alifika hospitali macho yake yakiwa yamenyofolewa na kubaki hukohuko,hospitali hakufika hata na mabaki ya goroli.
Akielezea kitaalamu Dokta Mataka alisema kwa kawaida mtu
anapotobolewa macho na kitu chochote ni lazima ukute goroli zikiwa
zimepasuka na utete wenye utelezi unakuwa umetapakaa machoni lakini kwa
majeruhi huyo goroli za macho yote mawili zilikuwa hazipo kabisa.
“Ukweli hiyo hali ilinishangaza sana kwa miaka 14 nikiwa kama
daktari bingwa wa macho sijawahi kukutana na tukio kama hilo hivyo baada
ya kupigwa na butwaa niliwapigia mabingwa wenzangu waje kujionea hali
hiyo na tushauriane jinsi ya kufanya.
“Hata wao walivyofika wote walishangaa na kuniambia nao hawajawahi kukutana na hali hiyo.
“Nilimtibia majeruhi wakati huo huo nilikuwa nikimuongelesha na
kumuuliza yaliyomsibu ambapo aliniambia wakati akinunua kuku pale
Buguruni ndiyo akatokea mtu na kuanza kumshambulia.
“Nikamuuliza kama anamfahamu hiyo mtu aliniambia akimuona atamtambua.
“Baada ya matibabu nilimpeleka wodini na kumuandikia tarehe za
kuhudhuria kliniki na nilimuambia kuwa katika maisha yake hawezi kuona
tena hivyo ajifunze kuishi maisha ya mtu asiye na macho.
“Baadae alipoanza kuja kliniki aliniambia kuwa mama yake alikuwa
akitaka kumpa jicho lake moja lakini nilimueleza ukweli kuwa hilo
haliwezekani.
“Huwezi kulihamisha jicho halafu likawa hai hiyo huduma haipo hapa duniani.
Baada ya kutoa ushahidi wake mbele ha Hakimu Frola Haule kesi hiyo
iliahirishwa mpaka Februari 22 mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani
hapo ambapo daktari bingwa wa tumbo ambaye nae alimtibu majeruhi huyo
anatarajiwa kutoa ushahidi wake kwa upande wa serikali.

0 comments:
Post a Comment