Posted by Williammalecela.com on Thursday, February 02, 2017
 |
Aliyekuwa mfungwa wa kisiasa nchini Gambia Ndg.Amadou Sanneh, mwenye
umri wa miaka 72 ameteuliwa kuwa Waziri wa fedha, ikiwa ni siku 3 tu
baada ya kuachiliwa huru na Rais Adama Barrow.
Amadou aliwekwa
gerezani na Rais Yahya Jammeh kutokana na kushiriki maandamano ya
kupinga utawala wake mwaka 2013. Tangu mwaka 1994 Rais Jameh aliposhika
madaraka, Amadou amekuwa mfungwa maarufu wa kisiasa kwa kukamatwa,
kuwekwa jela, na kuachiwa.
Amadou na viongozi wenzake watano wa
chama cha UDC walikamatwa mara ya mwisho mwaka 2013 ambapo walitupwa
gerezani kwa amri ya Rais Jameh na kuamuru kutumikia kifungo cha maisha.
Licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kama Amnesty
International kutaka waachiwe, lakini Rais Jameh aliendelea kushikilia
msimamo wake wa kutowaachia.
Amadou ni msomi wa masuala ya fedha
mwenye shahada ya Uhasibu na Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa biashara
(MBA). Ameshika nafasi mbalimbali za kisiasa ikiwemo kuwa mweka hazina
wa chama cha upinzani cha UDP kabla ya kuswekwa gerezani mwaka 2013.
Amadou aliachiwa huru jumatatu January 30 mwaka huu, na siku 3 baadae
ameteuliwa kuwa Waziri wa fedha wa nchi hiyo. Shirika la habari la ABC
limeripoti habari ya kuachiwa Amadou na kuteuliwa kuwa Waziri kama
mafanikio makubwa ya demokrasia kupitia taarifa yenye kichwa "From Jail
to Cabinet Minister; Gambia's New Government Forms" |
0 comments:
Post a Comment