Posted by Williammalecela.com on Tuesday, April 04, 2017
![[IMG]](https://lh3.googleusercontent.com/blogger_img_proxy/AEn0k_tZBUOijjk2SiSux4GJHFJJMGno0a7LPUHAfMfdWH-5msbTv0poxR1i_lvXijebyXRddAyxwGJkd23C4E4V3w0U9hlxYYa_Fh5RnJAxabGKgi1dGJbwfzgHLjXRtdAXgR1U98wc84Fd49exG8HMAukJ=s0-d)
=======
Prof. Kitila Mkumbo: Historia yake
View attachment 490978
Prof. Kitila Mkumbo ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam na
mwanaharakati wa masuala ya kisiasa. Alizaliwa tarehe 21 Juni 1971
katika Kijiji cha Mgela wilayani Iramba, Singida. Prof. Kitila hakuwa na
bahati ya kulelewa na wazazi, hivyo alisomeshwa kwa misaada ya ndugu na
wasamaria wema.
Alisoma katika Shule ya Msingi Mgela iliyoko wilaya ya Iramba kati ya
mwaka 1981-1987 kisha akajiunga Shule ya Sekondari Mwenge (Singida) na
kusoma kidato cha kwanza hadi cha tano mwaka 1988-1991 na elimu ya Juu
ya Sekondari akaipata pale Shule ya Sekondari Pugu kati ya mwaka
1992-1994 akijikita katika mchepuo wa PCB (Fizikia, Kemia na Bailojia).
Baada ya kuhitimu kidato cha sita alifanya kazi ya kuvua samaki katika
Bwawa la Mtera huko Iringa kwa sababu ya kuwa na hali mbaya ya kiuchumi
na baadaye alipata nafasi ya kwenda kujiunga na mafunzo ya polisi kwenye
Chuo cha jeshi CCP Moshi kwa muda wa miezi miwili lakini alikatisha
mafunzo baada ya kuchaguliwa kujiunga Chuo Kikuu.
Prof. Kitila alihitimu shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar Es
Salaam mwaka 1999 akisomea Sayansi ya Elimu akaanza kazi hapo hapo Chuo
Kikuu kama Ofisa Utawala, aliifanya kazi hiyo kwa miaka minne (1999 –
2003) na wakati anafanya kazi aliendelea kusoma shahada ya
uzamili/umahiri (M.A) akibobea katika Saikolojia, alihitimu shahada hiyo
mwaka 2002.
Kitila alifanya vizuri katika shahada ya umahiri na baada ya kufundisha
Chuo Kikuu kwa miaka michache alipewa udahili katika Chuo Kikuu cha
Southampton kilichoko nchini Uingereza ambako alitunukiwa shahada ya
uzamivu akibobea pia katika saikolojia, hii ilikuwa ni mwaka 2008.
Kati ya mwaka 2009 – 2012, Prof. Kitila amefanya kazi kama mratibu wa
kamati ndogo ya ufundi ya masuala ya UKIMWI lakini pia kuanzia mwaka
2010 hadi hivi sasa ameendelea kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya
TCIB (Tanzania Citizens Information Bureau (TCIB).
Mwaka 2010 hadi 2012 amekuwa Makamu Mwenyekiti wa UDASA (Jumuiya ya
Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam) na kisha akachaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa UDASA Oktoba 2014 na anaendelea na wadhifa huo.
Mwaka 2009 alikuwa Ofisa anayesimamia mitihani katika Shule ya Elimu ya
Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam, amekuwa mhariri mkuu na mhariri msaidizi
wa machapisho mbalimbali yanayohusu elimu ya saikolojia, sanaa na
sayansi.
Pia, amekuwa mkuu wa Idara ya Elimu ya Saikolojia na masomo ya Mtaala
katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaama kuanzia mwaka 2009 – 2012, amekuwa
Mhadhiri Mwandamizi kuanzia mwaka 2011 – 2014, amekuwa Mkuu wa Kitivo
cha Elimu katika Chuo Cha Elimu cha Dar Es Salaam (DUCE) na kufanikiwa
kuwa Profesa Mshiriki katika Shule ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar Es
Salaam kuanzia Julai 2014.
Kitila alianza siasa kama mwanachama wa CCM, baadaye alijiunga CHADEMA
kawa mshauri muhimu wa chama hicho. Naweza kuthubutu kusema, kati ya
wasomi na wataalam waliotoa mchango mkubwa kiushauri, kiuhaulishaji na
kimkakati na kuifanya CHADEMA iwe chama kinachojiendesha kisasa sana leo
hii, mmoja wa wasomi hao ni Prof. Kitila.
Mwaka jana (2014), Prof. Kitila alifukuzwa katika chama chake cha zamani
(CHADEMA) kwa tuhuma za kuandaa waraka wa mapinduzi na kukihujumu chama
hicho, Kitila alitangaza kuwa angeshirikiana na wenzake kuanzisha chama
kipya ambacho hivi sasa kinajukana kama ACT – Wazalendo. Na hata rafiki
yake wa siku nyingi, Zitto Kabwe amekweishjiunga na chama hicho. Hata
katika chama hiki kipya yeye amekuwa mshauri mkuu. Watu nilioongea nao
kutoka ndani ya ACT wanasisitiza kuwa Kitila ana mchango mkubwa na
unaoonekana anapokuwa katika taasisi yoyote ile.
Prof. Kitila amekwishafanya tafiti zaidi ya 18 na zimechapishwa katika
majarida ya kitaaluma ya kimataifa, amekwishaandika vitabu takribani
vitatu, ameoa na ana watoto watatu.
MBIO ZA UBUNGE
Prof. Kitila hakuwahi kugombea ubunge katika jimbo lolote hapa Tanzania,
muda wake mwingi amejikita katika masuala ya kitaaluma na ushauri wa
mikakati ya kisiasa. Japokuwa alipokuwa mwanachama hai wa CHADEMA
alifanya harakati nyingi katika jimbo la Iramba, (jimbo linaloongozwa na
Mwigulu Nchemba wa CCM) na amewahi kuingia kwenye misukosuko mingi na
hata kufunguliwa kesi ya kisiasa kwa sababu ya harakati zake.
NGUVU YAKE
Sifa na nguvu ya kwanza ya Prof. Kitila ni kuwa kijana na msomi mahiri.
Pamoja na kuwa wasomi wengi wanapewa madaraka na wanavurunda kama vile
hawakwenda shule, bado mataifa yote duniani hayakwepi wala kukimbia
dhana ya kuongozwa na watu walioelimika maana kuna wasomi wengi tu ambao
ni waadilifu sana katika kazi zao, mmoja wao ni Prof. Kitila.
Ukiniuliza mmoja kati ya wasomi wanaojua majukumu yao na wanayasimamia
sana, ntakwambia Prof. Kitila ni mmoja wao. Nguvu na sifa hii vina maana
kubwa sana kwa mtu ambaye anafikiri au anafikiriwa kuwa rais wa nchi.
Lakini jambo la pili, yeye ni mwanademokrasia thabiti na anayependa
demokrasia iwe katika vitendo. Msomi huyu ni mmoja wa watu wanaoamini
katika kujenga hoja na wanaopenda hoja zishindanishwe na zijadiliwe kwa
uwazi na kisha hoja yenye mashiko ndiyo ipitishwe na kukubaliwa na pande
zote kwa sababu ina tija kwa jamii au taifa.
Ukitembelea ukurasa wake wa “Facebook” utaona watu wanaandika jambo
lolote na humuoni akigombana nao, anapingwa waziwazi na wakati mwingine
anatukanwa lakini anaacha uhuru wa wanaompinga na kumtukana uendelee.
(Mimi binafsi nimekuwa sipendi mtu anitukane au anidhalilishe kwenye
mitandao, napenda kupingwa kwa hoja na si kutukanwa, na nakumbuka kila
aliyenitukana niliishia kumuondoa miongoni mwa marafiki).
Prof. Kitila yeye ameenda mbali zaidi, yuko tayari kwa hoja na yuko
tayari hata kutukanwa na kudhalilishwa, mwisho wa siku kila mtu
huendelea kuwa rafiki yake kwa muktadha huo. Sifa hii ni ngumu mno
kuipata kwa wanasiasa wengi, uvumilivu wao una ukomo lakini kwa Kitila
ni tofauti. Nchi kama yetu inahitaji watu wa namna hii kwenye uongozi wa
juu.
Jambo la tatu ambalo ni nguvu na sifa ya Prof. Kitila ni kubahatika kuwa
kiongozi kila alipokaa, kusoma, kufanya kazi n.k. Amebahatika kuwa
kiongozi tokea akiwa mdogo, nidhamu na kuwajali wenzake viliwavuta watu
waliomzunguka kumtumia yeye awe mwakilishi wao. Amekuwa “kiranja” tokea
akiwa Shule ya Msingi, Sekondari na Sekondari ya Juu. Uwezo huu wa
kiuongozi uliendelea hata alipokuwa Chuo Kikuu (UDSM) kwani alichaguliwa
kuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO) kati ya mwaka 1998 – 1999.
Watu nilioongea nao kuhusu uongozi wa Kitila alipokuwa DARUSO
wananiambia alikuwa na karama za kipekee. Mmoja ambaye hivi sasa ni
kiongozi mkubwa CCM na aliwahi kumpinga Kitila walipokuwa Chuo Kikuu,
amenieleza kuwa Kitila alikuwa na ushawishi mkubwa kila akisimama mbele
ya wanafunzi, hata kama mambo yalikuwa yemeharibika sana yalitengemaa.
Kitila ni mmoja wa Marais wa DARUSO waliovuka vikwazo vya kutopinduliwa,
watu waliowahi kuongoza DARUSO wanajua namna ilivyo rahisi sana kulala
ukiwa Rais wa wanafunzi na ukaamka ukiwa Mwanafunzi wa kawaida.
UDHAIFU WAKE
Moja ya mambo ambayo nayatizama kama udhaifu mkubwa wa Prof. Kitila ni
uthubutu unaopita kiasi. Binadamu waliofanikiwa huthubutu kufanya mambo
kadha wa kwadha lakini uthubutu kwa kiwango kisicholeta madhara
kulingana na mahali walipo. Jambo hili halifanywi na Kitila na mara
kadhaa amethubutu kufanya mambo yaliyowagutusha wenzie.
Mathalani, alipokuwa mwanachama wa CHADEMA alikiri kuhusika katika
kuandaa waraka uliopewa jina maarufu la “waraka wa mapinduzi ndani ya
CHADEMA”. Waraka ule ulikuwa ni moja ya mikakati ya msomi huyu kumpigia
chapuo rafiki yake wa siku nyingi “Zitto Kabwe” ili ajiandae kuongoza
chama hicho kupitia kwenye uchaguzi uliokuwa ukifuata. Waraka wa Kitila
na wenzake ulitafsiriwa kama njama za mapinduzi ndani ya chama, usaliti
na “kitu kisichofaa”.
Uthubutu huu wa Kitila ungewezekana sana kama angekuwa anafanya kazi
katika vyama vikubwa mno duniani, siyo hapa Afrika Mashariki, tena
nchini Tanzania. Lazima tukubali kuwa vyama vya kiafrika vimejijenga
katika mifumo migumu sana kuingilika kidemokrasia na mara nyingi vina
shida kwenye eneo hilo, ndiyo maana nilishtushwa na kujua kwamba Kitila
amekubali kuhusika na waraka ule wakati anatambua kuwa yuko Afrika
ambako demokrasia inapiganiwa kwa matakwa ya walioko madarakani kwa
wakati husika.
Kwa siasa za Afrika, hata huko ACT ambako Kitila ni mwanachama leo hii,
ukijaribu kuandaa waraka kama ule wa CHADEMA, nako unaweza kuonekana
kama Msaliti, mfanya mapinduzi, mhaini n.k. Ndiyo maana nasisitiza kuwa
uthubutu huu unaopitiliza ni tatizo kubwa sana kwake na kwa watu
waliomzunguka na tamaduni zao. Hata akiwa Rais wa nchi atazungukwa na
watu mbalimbali, aliowakuta na watakaomkuta, atakuwa na jukumu la
kufanya mambo kwa uthubutu wa viwango vinavyokubalika ndani ya taasisi
aliyomo kuliko “kuthubutu kulikovuka mipaka” ambako kunatizamwa kama
uhaini kwa tamadani na demokrasia ya Afrika.
Lakini kuthubutu huku kulikopitiliza ndiko pia kumemfanya Kitila mara
kadhaa atofautiane sana na menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam
kwenye mambo kadha wa kadha. Ubishi, na kutokukubali mambo kirahisi au
kutokukubaliana na mazingira na tamaduni za mahali ulipo, ni mambo
ambayo yanamgharimu sana na nayatizama kama madhaifu yatakayoendelea
kutishia ustawi wake kisiasa.
Mchambuzi ni Julius Mtatiro, Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB (Student): juliusmtatiro@yahoo.com, +255787536759.
0 comments:
Post a Comment