Kimenuka! Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma
linamshikilia Musa Moyo (40) wa Kijiji cha Mbangamawe wilayani Songea
mkoani hapa kwa tuhuma za kuwauzia nyama ya mbwa majirani zake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma,
Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilijiri Januari 12, mwaka huu
katika kijiji hicho ambapo inadaiwa Moyo alikamatwa na afisa mtendaji wa
kijiji hicho, Theopista Komba.
Kamanda Malimi alisema siku ya tukio,
afisa mtendaji huyo alipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa, Moyo
anafanya biashara ya kuuza nyama ya mbwa kwa matumizi ya binadamu.
Alisema mtendaji huyo alilazimika
kufuatilia tukio hilo kwa kina ambapo alikwenda nyumbani kwa Moyo
akijifanya mteja wa nyama hiyo kwa ajili ya kitoweo.
Alisema,
Moyo alimuuzia Komba nyama kidogo iliyokuwa imebaki ndipo mtendaji huyo
alipomkamata na nyama hiyo iliyokuwa imekaushwa na kukatwa vipande.
Afande Malimi alisema Moyo alifikishwa
kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Mjini Songea na kufanyiwa mahojiano ambapo
alikiri nyama hiyo ni ya mbwa aliyemchinja siku moja kabla ya
kukamatwa.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa
ya Songea alithibitisha kuwa, nyama hiyo ni ya mbwa ingawa jeshi la
polisi likiendelea kufanya uchunguzi na kuwataka wananchi kuacha mara
moja kununua nyama mitaani.
0 comments:
Post a Comment