IMEELEZWA kuwa matatizo ya uzazi yapo zaidi kwa wanaume kuliko kwa wanawake tofauti na inavyodhaniwa na watu wengi.
Daktari
bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake ambaye pia alikuwa Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Udaktari kabla ya kuwa Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), ambaye hivi sasa
ni mstaafu, Profesa Malise Kaisi alisema hayo katika mahojiano maalum
na HabariLeo, jijini Dar es Salaam.
Profesa
Kaisi alifafanua kuwa, mara nyingi wanawake aliowafanyia tiba ya
matatizo ya ugumba ni wale ambao waume zao walikuwa na kasoro katika
uwezo wao wa kuzaa na si wao. “Hapa nina maana kuwa mara nyingi watu
tuliowafanyia tiba hii ni wale ambao waume zao walikuwa na kasoro katika
uwezo wao wa kuzaa.
“Ushauri
katika matatizo ya uzazi ni lazima watu wote wahusishwe si wanawake
pekee. Uchunguzi tulioufanya Muhimbili ulionesha kuwa katika kila ndoa
10 zenye matatizo ya uzazi, ndoa nne tatizo lilikuwa kwa mwanamke na nne
tatizo lilikuwa kwa mwanamme. Ndoa mbili zilizobaki tatizo lilikuwa
pande zote, lakini zaidi kwa wanaume, kuliko wanawake,” alisema.
Alisema
mawazo yaliyojengeka kwa watu wengi kuwa matatizo ya uzazi yapo kwa
wanawake pekee si sahihi kwani katika tiba ya namna hiyo inashauriwa
wanandoa wote wafike kwa daktari na si mwanamke peke yake.Dk Kaisi
alisema mahusiano yasiyokuwa ya karibu katika ndoa yamewafanya kwa
kiwango kikubwa wanandoa wengi kutokupata watoto na hivyo kuingiwa na
hofu kuwa wana matatizo ya uzazi.Akifafanua hilo alitoa mfano kwa ndoa
moja kuwa kwa miaka saba tangu walipooana walikuwa hawajapata watoto
hivyo alipozungumza nao akabaini kuwa kazi wanazozifanya zimesababisha
wawe mbali muda mwingi.
“Unakuta
baba kazi yake ni kusafiri kila mara na mama naye hivyo, siku
wanapokutana inakuwa si siku sahihi kwao, matokeo yake wanalalamika kuwa
hawapati watoto kumbe ni elimu tu inatakiwa hapo.Baada ya kukutana na
wanandoa hao na kuwashauri haikupita muda wakapata watoto,” alisema.
“Tatizo
la elimu limekuwa ni sababu kubwa ya wanandoa kutoshika mimba. Maisha
ya sasa watu wapo mbiombio kutafuta fedha hivyo hawajui siku sahihi za
wao wanazostahili kukutana na kupata mtoto. Inawezekana hicho nacho ni
kisababishi.”
Alitaja
sababu nyingine zinazoweza kuchangia wanandoa kutopata watoto kuwa ni
chuki na mifarakano katika ndoa. Matatizo ya uzazi kwa wanawake Akina
mama wana matatizo mengi, mojawapo kubwa linalowasumbua ni tatizo la
kutokushika ujauzito.
Mwanamke
kushindwa kupata ujauzito kwa kipindi cha ndani ya mwaka mmoja au zaidi
ya mwaka mmoja wakati mwanaume na mwanamke wanakutana kwa muda
unaotakiwa na bila kutumia njia za kuzuia mimba ni tatizo.
Kuna
aina mbili ya tatizo hili moja hujulikana zaidi kwa jina la primary
infertility. Hii humaanisha kuwa mwanamke hajawahi kushika ujauzito
maishani mwake.
Pili
ni secondary infertility, hii humaanisha kuwa aliwahi kupata mimba
lakini ikashindikana kupata nyingine, na ya tatu ambayo hutokea mara
chache kama asilimia 20 hujulikana kama fecundability ambapo mwanamke
anakuwa na uwezekano wa kupata mimba ndani ya mzunguko mmoja wa hedhi.
Matatizo
ya uzazi kwa wanaume Ugumba kwa mwanaume, ni hali ambayo mwanaume
anashindwa kumpa mimba mwanamke, tatizo hili kwa mujibu wa takwimu
zilizopo huwaathiri wanaume kwa asilimia 40 hadi 50 na huwapata takriban
asilimia saba ya wanaume.
Ugumba kwa wanaume kwa kiasi kikubwa husababishwa na tatizo katika uzalishaji na utoaji wa mbegu za uzazi.
“Tunaposema
mwanaume ni mgumba ni pale ameishi na mwanamke kwa mwaka mmoja na tendo
la kujamiiana linaendelea kikamilifu lakini hatuoni matokeo. Ingawa
tatizo la uzazi lipo pande zote mbili kwa mwanamke na mwanaume, lakini
mwanaume pia ana asilimia kubwa ya kuwa na tatizo la uzazi kama ambavyo
tumekwishaona hapo awali.”
Tatizo
la uzazi linatokea kwa mtu yeyote bila kujali kama alishawahi kumpa
mimba mwanamke au kama ni mwanamke pia haijalishi kama alishawahi kupata
ujauzito siku za nyuma.
Mtu
anaweza kuwa na historia nzuri kuwa alishawahi kumpa mimba mwanamke
lakini linaweza kutokea tatizo akashindwa kusababisha ujauzito tena.
Chanzo
mojawapo katika sehemu hii ni matumizi ya baadhi ya madawa yawe ya
hospitali, ya asili au ya kulevya ambayo huathiri kwa kiasi kikubwa
uzazi na ndiyo maana inashauriwa unapokuwa na tatizo muone daktari kwa
uchunguzi zaidi na tiba.
Walevi
nao huathirika sana na matatizo ya uzazi kwani ulevi wa kupindukia
huathiri utendaji wa tendo la kujamiiana na uzalishaji wa mbegu za
kiume. Kuendesha baiskeli mwendo mrefu na kwa muda mrefu pia ni mojawapo
ya vyanzo.
Matatizo
ya vinasaba nayo huchangia. Uvutaji wa sigara kwa mwanaume unaathiri
uzalishaji wa mbegu za uzazi kwa asilimia thelathini, kemikali zilizomo
kwenye tumbaku zimethibitishwa kuua mbegu za kiume ndiyo maana pamoja na
madhara mengi ya sigara ndiyo maana makampuni yanayotengeneza sigara
huweka onyo kwa wavutaji wa sigara kwamba ni hatari kwa maisha yao.
Aidha
aina ya mavazi yanayovaliwa na wanaume yanaweza kusabnabisha kiwanda
cha kutengeneza manii kuvia. Kiasili kiwanda cha kutengeneza manii
hutakiwa kuwa na joto la wastani na kutobanwa kwa muda mrefu.
IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI-HABARILEO
0 comments:
Post a Comment