Friday, June 9, 2017

 Image may contain: 1 person, standing and outdoor
BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2017/18
I. UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Bajeti hii inawasilishwa kwa kuzingatia matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 137 ikisomwa pamoja na Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 26.

2. Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina makadirio ya Bajeti kwa Mafungu. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 pamoja na Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Serikali wa mwaka 2017 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.

3. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18.

4. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini katika dhamana hii kubwa ya kuongoza wizara nyeti ya Fedha na Mipango. Aidha, ninamshukuru sana kwa kuniongoza na kunitia moyo pale mawimbi yalipozidi kuwa makubwa. Maneno yake mazito kwamba aliniteua ili nipigwe mawe badala yake na badala ya Watanzania maskini na kuwa nimtegemee Mungu daima, yamekuwa ndiyo nguvu yangu katika kazi. Vile vile, nampongeza Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Ruangwa kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya ya kutuletea maendeleo Watanzania wote.

5. Mheshimiwa Spika, naomba pia kuwapongeza viongozi wakuu wa mihimili ya dola, nikianza na wewe mwenyewe Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa jimbo la Kongwa, na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mbunge) Naibu Spika. Ninawapongeza kwa umahiri na busara zenu katika kuongoza Bunge hili. Vile vile, ninawapongeza kwa dhati Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma, Kaimu Jaji Mkuu, kwa kuongoza vyema mhimili wa mahakama katika kutoa haki.

6. Mheshimiwa Spika, ninawapongeza pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, nikianza na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo; Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro; Kamishna Jenerali wa Magereza, Dkt. Juma Alli Malewa; Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala; Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Dkt. Modestus Kipilimba; Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola; Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers William Siang’a; na Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji Bw. Thobias Andengenye, pamoja na makamanda, askari na watumishi wote wa vyombo hivyo kwa uhodari wao katika kuilinda nchi yetu na kuhakikisha amani, usalama na uhuru wetu wa kisiasa na kiuchumi vinadumishwa.

7. Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapongeza Wabunge wapya walioingia katika Bunge hili mwaka huu wa fedha ambao ni Mheshimiwa Juma Ali Juma, Mbunge wa Dimani (CCM); Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare – Mbunge wa Viti Maalum (CCM); na Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA). Nawapongeza pia Waheshimiwa Wabunge walioteuliwa na Rais: Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb); Mheshimiwa Anne Kilango Malecela, (Mb); Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete (Mb); na Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria. Hongera sana kwenu nyote.

Sambamba na hilo, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge hili kuiwakilisha nchi yetu ya Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki ambao ni: Mhe. Fancy Nkuhi, Mhe. Happiness Legiko, Mhe. Maryam Ussi Yahya, Mhe. Dkt. Abdallah Makame, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe, Mhe. Mhandisi Habibu Mnyaa, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa, Mhe. Pamela Massay na Mhe. Josephine Lemoyani. Nawatakia kazi njema na kuwasisitiza wasiyumbe katika kusimamia maslahi ya kimkakati (strategic interests) ya Taifa letu katika mijadala ya Bunge hilo la Afrika Mashariki.

8. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa pole kwa Watanzania waliopatwa na majanga mbalimbali na misiba, nikianza na Bunge ambalo liliwapoteza wenzetu, Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir aliyekuwa Mbunge wa Dimani (CCM) na Mheshimiwa Dkt. Elly Marko Macha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA). Aidha, Bunge liliondokewa na Spika mstaafu, Mheshimiwa Samuel John Sitta, mzee wa kasi na viwango. Vile vile, natoa pole kwa wazazi na ndugu wa wanafunzi 32, walimu wawili na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vincent waliofariki kwa ajali ya gari tarehe 06 Mei, 2017 katika wilaya ya Karatu. Vivyo hivyo, ninatoa pole kwa ndugu wa askari wetu wanane na wananchi wengine ambao wameuwawa na kundi la kihalifu katika wilaya za Kibiti na Rufiji kwa nyakati tofauti katika mwaka huu. Mungu azilaze roho za marehemu wote hao mahala pema peponi. Amina!

9. Mheshimiwa Spika, ninawiwa kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na makamu wake Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa kupitia na kuchambua mapendekezo ya bajeti ninayowasilisha hivi sasa na kutoa maoni na ushauri uliochangia kuboresha Bajeti hii ya Serikali kwa mwaka 2017/18. Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kudumu za kisekta na waheshimiwa wabunge wote kwa ushauri na mapendekezo mliyotoa kwa Serikali wakati wa kuchambua Bajeti za kisekta. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2017.
10. Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Kondoa, ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa ushirikiano na msaada anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu ya wizara yangu. Aidha, napenda kumshukuru Bwana Doto M. James, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa usimamizi wa kazi za kila siku za wizara na uratibu mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii, akisaidiwa na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Dorothy Mwanyika, Bibi Amina Kh. Shaaban na Dkt. Khatibu Kazungu.
11. Mheshimiwa Spika, ninaendelea kumshukuru sana Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania kwa kuongoza kwa weledi taasisi hiyo nyeti yenye jukumu la kusimamia sekta ya fedha na kulinda utulivu na ukuaji wa uchumi wa Taifa. Aidha, napenda kutambua kazi nzuri ya viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika kukusanya mapato ya Serikali wakiongozwa na Bw. Charles Kichere, Kamishna Mkuu wa Mamlaka. Pia ninawashukuru Dkt. Oswald Mashindano, Msajili wa Hazina na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Vile vile, ninawashukuru Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara na vitengo vya Wizara, pamoja na watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kukamilisha Bajeti hii.

12. Mheshimiwa Spika, Bajeti hii pia imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo jumuiya ya wafanyabiashara na Washirika wa Maendeleo. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri. Kipekee niwashukuru wajumbe wa Kikosi Kazi cha Maboresho ya Mfumo wa Kodi (Task Force on Tax Reforms) ambayo inaundwa na wawakilishi wa sekta binafsi na wataalam wa kodi kutoka vyuo vikuu na taasisi za utafiti.
Aidha naishukuru Kamati ya Ushauri kwa Waziri wa Fedha kuhusu hatua za mapato (Advisory Committee on Revenue Measures). Uchambuzi na ushauri wao umechangia kufikia hatua mpya za kodi nitakazopendekeza hivi punde.

13. Mheshimiwa Spika, hotuba hii inawasilisha Bajeti ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali inaleta Bajeti hii kwa dhamira ya kuongeza kasi ya kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 – 2020; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/172020/21; Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

14. Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 11 tarehe 20/11/2015, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaeleza Watanzania kwamba, vipaumbele vya Serikali yake kuhusu uchumi ni kuendeleza na kuimarisha misingi imara ya uchumi wa nchi yetu iliyojengwa katika awamu za uongozi zilizotangulia. Vipaumbele hivyo ni vifuatavyo:

i. Kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio wengi yafananefanane na nchi ya kipato cha kati;

ii. Kuongeza mapato, kuziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, na kusimamia sheria za manunuzi ya umma;
iii. Ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi (barabara, reli, usafiri wa anga na wa majini, umeme) ili kushawishi na kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje;

iv. Kuhakikisha kwamba madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu;

v. Kuweka mkazo mkubwa na kusimamia uendelezaji wa viwanda kwa kutambua kwamba sekta binafsi ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Aidha, aina ya viwanda tunavyotaka ni vile ambavyo vina sifa ya kuzalisha ajira nyingi, sehemu kubwa ya malighafi husika itatoka ndani, na vile vya kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi nchini;

vi. Kuboresha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi, hususan kuongeza thamani na kuzifanya shughuli hizi kuwa za kisasa zaidi kwa kutoa mafunzo, pembejeo, zana na wataalam;
 

vii. Kuweka mkazo katika kuendeleza utalii, ardhi na utunzaji wa mazingira;

viii. Kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na umeme;

ix. Kupambana na tatizo kubwa la rushwa, ufisadi na madawa ya kulevya; na

x. Kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji serikalini ili kupunguza urasimu. Hivyo, mapitio ya mwenendo wa uchumi wa Taifa na tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika mwaka 2016/17 yamelenga kutoa picha ya utekelezaji wa vipaumbele hivyo vya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

15. Mheshimiwa Spika, katika hotuba niliyosoma leo asubuhi, nilieleza kwa kirefu hali ya uchumi wetu ilivyokuwa katika mwaka 2016 na miezi minne ya kwanza ya mwaka huu wa 2017. Inatosha nirejee kuwaambia Watanzania kwamba uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tano za Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi. Kwa mujibu wa takwimu za uchumi za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF World Economic Outlook Database), nchi hizo tano ni Ivory Coast (asilimia 7.9); Tanzania (asilimia 7.1); Senegal (asilimia 6.6); Djibouti (asilimia 6.5); na Ethiopia (asilimia 6.5).

Aidha, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani Bw. Tao Zhang alipotembelea Tanzania kwa mara ya kwanza mwezi Mei 2017, alitoa tathmini yake kwamba uchumi wa Tanzania umebaki kuwa imara kutokana na maboresho ya kisera yaliyotekelezwa chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hasa katika maeneo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

16. Mheshimiwa Spika, jarida la Benki ya Dunia (Tanzania Economic Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha waziwazi kuwa uchumi wa Taifa ni imara kwa kuangalia viashiria mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara, akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi, na naomba kunukuu kwa kiingereza:

“Tanzania’s economic performance continues to rank among the highest in the region. The real GDP growth rate has consistently outpaced its EAC peers. The inflation rate remains relatively low. The current account deficit has significantly improved, with gross reserves sufficient to cover four months of imports. The shilling has also remained stable in 2016, following significant depreciation and volatility in 2015.”

17. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo, pamekuwa na maeneo ambayo yametawala mijadala kuhusu afya ya uchumi wa Taifa, ambayo napenda kuyaelezea kwa kifupi. Maeneo hayo ni pamoja na ukwasi katika uchumi, kufungwa kwa biashara, na madai kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na kujiamini (private sector confidence) kutokana na baadhi ya hatua zilizochukuliwa na serikali bila ushirikishwaji wa wadau.
Hali ya Ukwasi Katika Uchumi

18. Mheshimiwa Spika, ukwasi ni kiasi cha fedha kilichopo katika uchumi kinachojumuisha fedha taslim zilizoko kwenye mzunguko nje ya mabenki na rasilimali fedha nyingine ambazo zinaweza kubadilishwa na kuwa fedha taslimu bila kikwazo. Utoshelevu wa ukwasi katika uchumi hupimwa kwa viashiria mbalimbali vikiwemo ujazi wa fedha, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi, kiwango cha mitaji ya mabenki, uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi na upatikanaji wa huduma za kifedha.

19. Mheshimiwa Spika, katika kipindi kilichoishia mwezi Machi 2017, hali ya baadhi ya vigezo vya ukwasi inaonyesha kuwa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ambao unajumuisha sarafu na noti zilizoko katika mzunguko nje ya mabenki, amana za muda mfupi, muda maalum na amana katika fedha za kigeni zilizopo katika mabenki, uliongezeka na kufikia shilingi trilioni 22.53 kutoka shilingi trilioni 21.65 katika kipindi kama hicho mwaka 2016, sawa na ongezeko la asilimia 4.1. Aidha, sekta ya kibenki iliendelea kuwa imara na himilivu, ikiwa na viwango vya mitaji na ukwasi ulio juu ya ukomo unaohitajika kisheria kama ifuatavyo: kwa kutumia kigezo cha uwiano kati ya mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslim na amana zinazoweza kuhitajika kwa muda mfupi (Liquid Assets to Demand Liabilities), uwiano huu ulikuwa asilimia 35.9 mwezi Machi 2017 ikilinganishwa na uwiano wa chini unaohitajika kisheria wa asilimia 20. Vile vile, uwiano wa mtaji wa msingi na rasilimali za benki ulikuwa asilimia 19.0 ambao uko juu ya kiwango cha chini kinachohitajika kisheria cha asilimia 10. Kadhalika, amana za wateja katika benki za biashara ziliongezeka kwa asilimia 0.3 kutoka shilingi trilioni 18.84 mwezi Machi 2016 hadi shilingi trilioni 18.89 mwezi Machi 2017.
20. Mheshimiwa Spika, takwimu pia zinaonesha kuwa ukwasi wa mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi 2017 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika cha asilimia 5. Mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi cha mwaka ulioishia Machi 2017 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2016. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara duniani ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania. Napenda kuchukua fursa hii kuyataka mabenki yote nchini kusimamia sawasawa taratibu za kibenki katika utoaji wa mikopo.

21. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua ikiwa ni pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara na hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu zaidi. Riba hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi tarehe 6 Machi 2017.
Aidha, katika kuimarisha zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama dhamana (Statutory Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0 ili kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta binafsi. Hatua hii imeanza kutumika rasmi mwezi Aprili 2017. Ni matumaini ya Serikali kuwa hatua hizi zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza ukwasi wa kutosha kuwakopesha wananchi kwa riba nafuu.

22. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, mwaka 2016/17 benki tatu za biashara zilifungwa kutokana na sababu mbalimbali. Benki hizo ni Benki ya Twiga, FBME Bank Limited; na Mbinga Community Bank. Mnamo tarehe 28 Oktoba 2016, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua usimamizi wa benki ya Twiga baada ya kubaini kuwa benki hiyo ilikuwa na upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huu wa mtaji ulionekana kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha na pia kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki ya Twiga kungehatarisha usalama wa amana za wateja wake. Hata hivyo, baada ya kukamilika kwa zoezi la kutathmini hali ya kifedha ya benki hiyo, Serikali iliruhusu baadhi ya huduma za benki hiyo ziendelee huku ikiendelea na mchakato wa kupitia na kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji linaloikabili benki ya Twiga. Kwa sasa Serikali inapitia maombi yaliyoletwa na wawekezaji mbalimbali wanaotaka kununua hisa na kuongeza mtaji wa benki hiyo.

23. Mheshimiwa Spika, tarehe 8 Mei, 2017 Serikali ilisimamisha shughuli zote za FBME Bank Limited; kufuta leseni yake ya kufanya shughuli za kibenki; kuiweka chini ya ufilisi; na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu ulifikiwa kutokana na mwelekeo wa benki hiyo kuwa mashakani kufuatia mahakama ya Marekani kukubaliana na ombi la Taasisi ya Marekani ya Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (FinCEN) la kuifungia FBME kutumia mfumo wa kibenki wa Marekani kutokana na tuhuma za kujihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha haramu. Naomba tena kupitia hotuba hii ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 kuyaonya mabenki yote yatakayobainika kujihushisha na biashara ya utakatishaji fedha haramu au kufadhili ugaidi au kwenda kinyume na sheria za nchi kwamba Serikali itachukua hatua kali za kufuta leseni za kufanya shughuli za kibenki hapa nchini mara moja na hatua
nyingine kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake, na hata sheria za kimataifa.


24. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania ilichukua hatua nyingine ya kuifunga MbingaCommunity Bank Plc, kusitisha shughuli zake zote za kibenki na kufuta leseni yake ya biashara ya kibenki kuanzia tarehe 12 Mei, 2017. Benki hiyo iliwekwa chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi. Uamuzi huu ulichukuliwa baada ya Serikali kujiridhisha kuwa MbingaCommunity Bank Plc ina upungufu mkubwa wa mtaji na ukwasi kinyume na matakwa ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huu wa mtaji na ukwasi ungeweza kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha, na wa amana za wateja. Serikali inapenda kuuhakikishia umma wa Watanzania kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki yaliyopo nchini kwa lengo la kulinda utulivu katika sekta ya fedha.

25. Mheshimiwa Spika, wigo wa utoaji huduma za kifedha kwa wananchi walio wengi zaidi na kwa gharama nafuu umepanuka sana kutokana na mtandao mkubwa wa mabenki na taasisi nyingine za fedha zipatazo 64 [benki za biashara 40, benki za maendeleo 3, benki za jumuiya 11, huduma ndogo za kifedha – (micro finance) 5, taasisi zinazotoa mikopo binafsi (private credit) 2, na kampuni za huduma za kifedha za kukodisha (lease finance) 3]. Sambamba na hizi, kuna huduma za kifedha na malipo kupitia huduma za benki zinazohamishika (mobile banking), mawakala na simu za mkononi. Hivi sasa, inakadiriwa kuwa Watanzania zaidi ya milioni 17 wanafanya miamala kwenye mfumo wa malipo kupitia simu za mkononi.

Kufungwa kwa Biashara

26. Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo lilikuwa likizungumzwa sana na wananchi na pia hapa Bungeni ni kuhusu kuongezeka kwa kasi ya kufunga biashara hususan, eneo la Kariakoo katika Jiji la Dar es salaam na katika miji mingine. Kwa mujibu wa taarifa zilizofikishwa TRA, katika kipindi cha kuanzia Julai 2016 hadi Machi, 2017 jumla ya biashara 7,277 zilifungwa katika mikoa mbalimbali nchini. Mwenendo huu kwa ujumla siyo mzuri kwa sababu wananchi wanapoteza ajira na kipato, Serikali inakosa mapato ya kodi na uchumi unadorora. Hivyo, ni muhimu pale wimbi la kufungwa kwa biashara linapotokea jitihada zifanyike kuelewa aina gani za biashara zinafungwa, kwa nini zinafungwa na hatua gani zichukuliwe kudhibiti hali hiyo.

27. Mheshimiwa Spika, ziko sababu nyingi zinazoweza kuwa zimepelekea hali hiyo, ikiwa ni pamoja na ushindani mkali wa kibiashara; usimamizi dhaifu wa biashara; kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara kama vile usafirishaji, kodi na tozo mbalimbali; na kutozingatia masharti ya kufanya
biashara. Lakini pia, imedhihirika kwamba, wafanyabiashara wengi wameanza mazoea ya kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mapato mara wanapofunga biashara zao. Hii ilitokana na elimu iliyotolewa na Mamlaka kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa ambazo zimewafanya walipa kodi kufahamu kuwa unapofunga biashara bila kutoa taarifa, kodi inajilimbikiza na wataendelea kudaiwa na TRA.


28. Mheshimiwa Spika, ni vema kutambua kwamba kufunguliwa au kufungwa kwa biashara ni jambo la kawaida kabisa katika uendeshaji wa biashara. Napenda kuliarifu Bunge hili kuwa, katika kipindi hicho hicho cha Julai 2016 mpaka Machi 2017, Mamlaka ya Mapato ilisajili biashara mpya zipatazo 224,738. Hivyo, picha inayotolewa isiwe ya upande mmoja tu. Ni vema pia kujua kwamba kufungwa kwa biashara sio kwa Tanzania pekee. Ni jambo ambalo linatokea katika vipindi mbalimbali katika historia za mataifa na kwa viwango tofauti tofauti. Watu wengi miongoni mwetu tumesoma kuhusu anguko kuu la biashara lililotokea katika bara la Ulaya na Amerika kati ya mwaka 19291939 likijulikana kama “the Great Depression”.

Huko China nako katika miaka 1980 biashara nyingi zilipigwa na dhoruba ambapo baadhi zilizama lakini nyingine ziliendelea kukua. Haya yameelezwa vizuri sana katika kitabu cha Tian Tao na wenzake kinachoitwa Huawei: Leadership, Culture and Connectivity kilichochapishwa mwaka 2017. Naomba kunukuu kwa lugha ya kiingereza kutoka ukurasa wa 43 wa kirumi wa kitabu hicho:

“From the 1980s onward, China was swept up in the largest wave of commercial development in human history. Businesses at the time were like ships, each raised up and carried along by the sheer momentum of the wave. Some, however, soon capsized and were swallowed up, while most drifted along, going with the flow. Others crashed against barriers in the sea or got stranded on deserted islands. Only a few rose atop the crest of the wave and survived, eventualy sailed towards new lands.”

29. Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara yangu inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara nchini na itachukua hatua stahiki itakapobidi kufanya hivyo. Wito wa Serikali kwa wafanyabiashara nchini ni kwamba fanyeni biashara zenu bila hofu kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za nchi.
Madai ya Kuwa Sekta Binafsi Imepoteza Kujiamini (Private Sector Confidence)

30. Mheshimiwa Spika, yamekuwepo madai ya kuwa wafanyabiashara wamepoteza kujiamini kutokana na matamshi ya viongozi na hatua zilizochukuliwa na Serikali bila kuwashirikisha wafanyabiashara ambazo zimezua hofu.

Napenda niwahakikishie wafanyabiashara kuwa, Serikali ya awamu ya tano inaamini kwa dhati kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi na inathamini sana na kupongeza mchango mkubwa sana wa wafanyabiashara katika uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kwa ajili ya matumizi nchini na mauzo nje yanayotupatia fedha za kigeni unafanywa na sekta binafsi. Lakini pia sekta binafsi ndiyo mwajiri mkuu na chanzo kikuu cha mapato ya Serikali. Hivyo, sekta binafsi ndiyo mbia mkuu wa Serikali katika kazi ya kuharakisha maendeleo nchini.

31. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa sekta binafsi na wafanyabiashara, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kujenga mazingira mazuri ya kufanya biashara. Katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, Serikali iliendelea na jitihada za kuimarisha utulivu wa uchumi jumla, kupunguza urasimu, kuharakisha maamuzi, kuimarisha ulinzi na usalama na kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu imara na huduma bora zikiwemo umeme wa uhakika na mikopo kwa sekta binafsi. Hayo yote ni maeneo ambayo Serikali iliyapa na itaendelea kuyapa kipaumbele. Aidha, Serikali bado ina dhamira ya dhati kuendeleza mashauriano na wafanyabiashara kupitia utaratibu wa mikutano ya Baraza la Taifa la Biashara, Taasisi ya Sekta Binafsi na makongamano mengine.

32. Mheshimiwa Spika, tumeanza kuona viashiria bora zaidi katika eneo hili la kuboresha mazingira ya biashara. Taarifa ya Benki ya Dunia ya mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya 132 kwa urahisi wa kufanya biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12 kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016. Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya “Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016” (Africa Investment Index, 2016) iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global Research Lab” ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.

33. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzungumza na wafanyabiashara ili kupata maoni na ushauri wao kuhusu sera mbalimbali na mwenendo wa uchumi kwa ujumla na kutatua kero zao. Nia ya Serikali ni kuhakikisha wanafanya biashara katika mazingira mazuri yanayotabirika ili biashara hizo zikue na kushamiri, ajira ziongezeke na Serikali ipate kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo na huduma za jamii. Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania itaendelea kuboresha mfumo wa kodi na kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kufanya biashara zao kwa urahisi. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali itaendelea na jitihada za kuelimisha umma juu ya umuhimu wa kurasimisha shughuli zao za kiuchumi. Pamoja na kutoa elimu, napenda kusisitiza kuwa, kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia kwa maendeleo ya Taifa. Lazima Watanzania tulipe kodi. Serikali hii haitavumilia uporaji wa rasilimali za nchi na ukwepaji kodi kwa kivuli cha kulinda imani (confidence) ya wafanyabiashara.

34. Mheshimiwa Spika, napenda nitumie pia fursa hii niwakumbushe watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwamba, kodi zinatozwa kwa kuongozwa na sheria na kanuni zake. Matumizi ya vitisho na unyanyasaji kwa walipa kodi, kuwadai rushwa au kuwazidishia makadirio ya kodi ili kuwakomoa ni mambo ya hovyo na hayakubaliki hata kidogo! Wale watumishi wa TRA, ambao naamini ni wachache tu, wanaojihusisha na vitendo hivyo, wakome kabisa kufanya hivyo. Wale tutakaowabaini tutawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma. Aidha, natoa rai kwa wafanyabiashara wetu na wananchi wazalendo kutupatia taarifa za ukweli kuhusu mwenendo mbaya wa mtumishi yeyote wa TRA ili zifanyiwe kazi na Serikali. Nawaomba pia mfanye hivyo hivyo kutupatia taarifa kuhusu wafanyabiashara wanaokwepa kodi ili tuwashughulikie ipasavyo.

II. TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2016/17
Mapato

35. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai 2016 hadi Aprili 2017, mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia shilingi bilioni 20,710.5, sawa na asilimia 70.1 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 29,539.6. Mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:

i. Mapato ya kodi yalifikia shilingi bilioni 11,644.6 sawa na asilimia 77.1 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 15,105.1;

ii. Mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi bilioni 1,611.0 sawa na asilimia 59.8 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 2,693.0;
iii. Mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalikuwa shilingi bilioni 399.3 sawa na asilimia 60.0 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 665.4 kwa mwaka;

iv. Mikopo kutoka vyanzo vya ndani ilifikia Shilingi bilioni 4,715.6, sawa na asilimia 87.7 ya shilingi bilioni 5,374.3 zilizotarajiwa kukopwa kwa mwaka kutoka katika chanzo hiki; na

v. Misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka nje iliyopokelewa hadi Aprili 2017 ni shilingi bilioni 2,340.1 sawa na asilimia 65.0 ya lengo la shilingi bilioni 3,600.8 zilizoahidiwa na Washirika wa Maendeleo kwa mwaka 2016/17.

36. Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali ilipanga kukopa kiasi cha shilingi bilioni 2,100.9 kutoka kwenye vyanzo vya kibiashara ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo lakini haikuweza kukopa kutokana
na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri. Hata hivyo, Serikali inakamilisha majadiliano na wakopeshaji ambapo kiasi cha dola za Marekani milioni 500 kinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Juni 2017.

Kudhibiti upotevu wa mapato

37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti upotevu wa mapato. Katika kutekeleza azma hii, baadhi ya taasisi zimeanza kutumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato. Mfano, Halmashauri zinatumia Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato wa Serikali za Mitaa (Local Government Revenue Collection System LGRCS) na Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Dar es Salaam linatumia Mfumo wa Udhibiti wa Vyombo vya Moto Barabarani (Traffic Management System). Aidha, Serikali imekamilisha mfumo wa kielektroniki (Government ePayment Gateway SystemGePGs) utakaotumika katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Mfumo utasaidia Serikali kuwa na uhakika wa mapato ya nayokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa wakati na kurahisisha ulipaji wa kodi, tozo na ada mbalimbali. Aidha, tarehe 01 Juni, 2017 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alizindua Mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa mjia ya kielektroniki. Mfumo huo unalenga kupata taarifa sahihi za mlipakodi na mtoa huduma hususan makampuni ya simu, mabenki na televisheni.
Ukusanyaji wa Kodi ya Majengo

38. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu inaipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa zote nchini kuanzia mwaka 2016/17. TRA ilipewa jukumu hili kutokana na kuwa na ufanisi katika ukusanyaji na mtandao mpana ulioenea nchi nzima. Uamuzi huu haukuwa na maana ya kupora chanzo hiki cha mapato kutoka katika halmashauri, bali kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi kutoka katika chanzo hiki.

39. Mheshimiwa Spika, baada ya kupitishwa kwa Sheria hiyo, hatua iliyofuata ilikuwa ni kutolewa kwa Tangazo la Serikali No. 276 la tarehe 30 Septemba 2016 lililoitaka TRA kuanza zoezi hilo kwa Halmashauri 30 za awali. Jukumu la kukusanya kodi ya majengo katika halmashauri zilizobaki liliendelea kubaki katika halmashauri husika. Katika kipindi hicho, Serikali kupitia TRA ilifanya maandalizi ya taratibu na mifumo ya ukusanyaji. Maandalizi hayo yalihusisha kutengeneza kanuni za ukusanyaji, kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa kodi hii, kuunda kitengo, kuweka wafanyakazi na vitendea kazi kabla ya kuanza ukusanyaji.
40. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa taratibu hizo, TRA ilianza rasmi kukusanya Kodi ya Majengo tarehe 1 Oktoba, 2016 katika majiji, manispaa na miji 30. Hadi Mei, 2017, TRA imekusanya jumla ya Shilingi milioni 15,134.2. Ni matumaini ya Serikali kwamba kwa mwaka 2017/18, TRA itafanya vizuri zaidi katika ukusanyaji wa kodi hii ya majengo. Maboresho ya kukusanya kodi hiyo nitayaeleza baadae. Natoa rai kwa wadau wote wakiwemo wamiliki wa majengo, viongozi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na Mamlaka ya Mapato Tanzania kushirikiana bega kwa bega kuhakikisha wanafanikisha zoezi hili la ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Matumizi

41. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Aprili, 2017 jumla ya shilingi bilioni 20,036.5 zilitolewa kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 15,480.9 zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 
87.4 ya lengo la mwaka na shilingi bilioni 4,555.5 zilitolewa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 38.5 ya lengo la shilingi bilioni 11,820.5 zilizotengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo kwa mwaka. Fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha fedha za ndani shilingi bilioni 3,647.7 na fedha za nje shilingi bilioni 907.8.

Hata hivyo, baadhi ya fedha za nje za kugharamia miradi ya maendeleo hazikujumuishwa kwenye matumizi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo: kuchelewa kupata thamani halisi ya vifaa vilivyopelekwa moja kwa moja kwenye miradi kutokana na baadhi ya Washirika wa Maendeleo kuendelea kupeleka fedha moja kwa moja kwenye miradi bila kupitia mfumo wa malipo wa Serikali.

42. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mahitaji yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha za matumizi ya maendeleo kati ya Julai, 2016 hadi Aprili, 2017 ni pamoja na:

i. Ujenzi na ukarabati wa barabara kuu za Mikoa na Halmashauri (Mfuko wa Barabara) shilingi bilioni 675.9;

ii. Miradi ya ujenzi wa barabara ikiwemo ulipaji wa madeni ya wakandarasi na wahandisi washauri shilingi bilioni 540.3;

iii. Miradi ya uzalishaji wa umeme, uboreshaji wa njia za kupitisha umeme na usambazaji wa umeme vijijini shilingi bilioni 421.5;

iv. Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu shilingi bilioni 393.2;

v. Malipo ya awali ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha ‘standard gauge’ awamu ya kwanza katika eneo la Dar – Morogoro (Km 205) shilingi bilioni 300;

vi. Ununuzi wa ndege mbili na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nne shilingi bilioni 234.9;

vii. Usambazaji wa maji mijini na vijijini shilingi bilioni 186.4; na

viii. Uboreshaji wa huduma za afya katika ngazi zote shillingi bilioni 170.6 ikiwemo ununuzi wa dawa na vifaa tiba shilingi bilioni 156.1.
 

43. Mheshimiwa Spika, utoaji wa fedha za matumizi ya kawaida unajumuisha shilingi bilioni 5,320.3, sawa na asilimia 80.6 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kugharamia mishahara; shilingi bilioni 7,775.5, sawa na asilimia 97.2 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa na shilingi bilioni 2,385.1, sawa na asilimia 76.5 ya lengo la mwaka kwa ajili ya kugharamia matumizi mengineyo.

44. Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyopewa kipaumbele katika utoaji wa fedha za matumizi mengineyo ni pamoja na:

i. Kugharamia shughuli za vyombo vya ulinzi na usalama shilingi bilioni 591.3;

ii. Elimu msingi bila malipo shilingi bilioni 203.0;

iii. Uendeshaji wa mitihani ya kitaifa shilingi bilioni 69.9;

iv. Mfuko wa Bunge shilingi bilioni 69.1;

v. Kugharamia balozi zetu nje ya nchi shilingi bilioni 68.7;

vi. Posho ya madaktari wanafunzi shilingi bilioni 15.3;

vii. Ruzuku ya pembejeo shilingi bilioni 15.0;

viii. Ruzuku ya vyama vya siasa shilingi bilioni 14.2; na

ix. Ununuzi wa chakula cha hifadhi ya Taifa shilingi bilioni 13.0.
Kudhibiti matumizi

45. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/17, Sera za Matumizi ya Serikali zililenga kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015, Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma SURA 348, Sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa SURA 290, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2013 SURA 410 na Kanuni husika, pamoja na miongozo mbalimbali ya Serikali. Lengo kuu lilikuwa ni kupunguza matumizi yasiyo na tija, kuziba mianya ya ufujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye maeneo ya kipaumbele.

46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/17 Serikali imeendelea kudhibiti matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo: kupunguza safari za nje kwa kuhakikisha kuwa vibali vinatolewa kwa safari zenye manufaa kwa Taifa; kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara; na kuendelea kudhibiti gharama za uendeshaji wa magari ikiwa ni pamoja na matengenezo, mafuta na vilainishi. Aidha, utaratibu wa kufanya mikutano na makongamano katika kumbi za Serikali na taasisi za umma umeongeza udhibiti wa matumizi ya Serikali.
Malimbikizo, uhakiki na ulipaji wa Madai

47. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Juni, 2016 madai yaliyokuwa yamewasilishwa na taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 2,934.4 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1,997.9 sawa na asilimia 68.1 zilithibitika kuwa madai halali baada ya uhakiki. Kati ya madai yaliyohakikiwa, Serikali
imelipa jumla ya shilingi bilioni 796.5 hadi mwezi Machi, 2017 na hivyo kubakia na madai ya shilingi bilioni 1,201.4. Kati ya madai hayo yaliyolipwa, shilingi bilioni 632.1 ni kwa ajili ya wakandarasi na wahandisi washauri; shilingi bilioni 78.9 kwa ajili ya wazabuni wa huduma na bidhaa ikiwemo shilingi bilioni 11.2 za Bohari Kuu ya Madawa (MSD); shilingi bilioni 67.6 kwa ajili ya malimbikizo ya madai ya watumishi; na shilingi bilioni 17.9 ni kwa ajili ya watoa huduma mbalimbali.


48. Mheshimiwa Spika, kati ya Julai hadi Desemba 2016, malimbikizo ya madai mapya kutoka kwenye taasisi mbalimbali yalikuwa jumla ya shilingi bilioni 899.55. Hivyo, hadi Desemba 2016, madai yote yalifikia shilingi bilioni 2,100.90. Madai hayo yamegawanyika kama ifuatavyo: shilingi bilioni 910.30 wakandarasi; shilingi bilioni 890.16 ni wazabuni wa huduma na bidhaa; shilingi bilioni 159.10 ni madai ya watumishi mbalimbali; shilingi bilioni 75.45 ni ankara za maji,umeme na simu; na shilingi bilioni 65.89 ni pango la ofisi. Aidha, kati ya madai ya wazabuni wa huduma na bidhaa, lipo deni la MSD ambalo ni shilingi bilioni 145.89 linalotokana na malimbikizo ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba vilivyochukuliwa na taasisi mbalimbali za serikali na havikuwa vimelipiwa.
Deni la Taifa

49. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Ili kuhakikisha kuwa deni la Taifa linaendelea kusimamiwa ipasavyo, Bunge lako Tukufu lilipitisha marekebisho ya Sheria hiyo mwezi Novemba, 2016. Baadhi ya maeneo yaliyorekebishwa ni pamoja na: kuongeza masharti kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yanayoomba dhamana ya Serikali ili kudhibiti utoaji wa dhamana hizo; kuweka utaratibu maalum wa kisheria ambao unahakikisha kwamba fedha zilizokopwa na Serikali ya Muungano kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo Zanzibar inafika kama ilivyokusudiwa; na kuongeza wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa.

50. Mheshimiwa Spika, Hadi Machi 2017, deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni 50,806.5. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni shilingi bilioni 42,883.6 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 7,922.9. Deni la Serikali limeongezeka kwa asilimia 9.2 kutoka shilingi bilioni 39,274.6 Machi, 2016 hadi shilingi bilioni 42,883.6 Machi, 2017. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na mikopo mipya na ya zamani iliyopokelewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 kutoka vyanzo vya masharti nafuu na ya kibiashara, malimbikizo ya riba ya deni la nje kwenye nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo zinatakiwa kutoa msamaha wa madeni lakini bado hazijatoa pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola za Marekani.

51. Mheshimiwa Spika, deni la Serikali linajumuisha deni la ndani la shilingi bilioni 12,073.7 sawa na asimilia 28.1 na deni la nje la shilingi bilioni 30,809.9 sawa na asilimia 71.9. Deni la nje linajumuisha mikopo ya masharti nafuu kutoka kwenye mashirika ya fedha ya kimataifa, sawa na asilimia 56.8, mikopo kutoka nchi wahisani ilifikia asilimia 16.3 na mikopo kutoka mabenki ya kibiashara ya kimataifa ilifikia asilimia 26.9 ya deni lote la nje. Mikopo hiyo ilitumika kugharamia miradi ya maendeleo hususan katika sekta za ujenzi (barabara na reli), nishati, uchukuzi, elimu na maji.

Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa

52. Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika mwezi Novemba, 2016 yalibainisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya Deni la Taifa (Present Value of Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56; thamani ya sasa ya Deni la nje (Present Value of External Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 250. Viashiria hivyo vinapima uwezo wa nchi kukopa bila kuathiri uhimilivu wa deni (solvency indicators).

53. Mheshimiwa Spika, kutokana na tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa, ambayo inapima uwezo wa nchi kulipa deni, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20. Kwa kuzingatia viashiria hivyo, ambavyo vipo chini ya ukomo unaokubalika kimataifa, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje.
III. SERA ZA BAJETI KWA MWAKA 2017/18

54. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, dhima ya Bajeti ya mwaka 2017/18 ni “kujenga uchumi wa viwanda utakao chochea ajira na ustawi endelevu wa jamii”. Hii inaendana na msisitizo na vipaumbele vya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kujenga Tanzania ya viwanda.
Shabaha za Uchumi Jumla

55. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 unalenga kufikia shabaha za uchumi jumla kama ifuatavyo:
 

i. Pato halisi la Taifa kukua kwa asilimia 7.1 mwaka 2017 kutoka asilimia 7.0 mwaka 2016;

ii. Kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei katika wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 5.0 na asilimia 8.0 mwaka 2017;

iii. Mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17, na kuendelea kuongezeka kufikia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18;

iv. Mapato ya kodi yanakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 13.3 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;

v. Matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka kufikia asilimia 

26.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18 kutoka matarajio ya asilimia 

23.7 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;

vi. Nakisi ya bajeti inatarajiwa kupungua kufikia asilimia 3.8 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 4.5 ya Pato la Taifa mwaka 2016/17;
vii. Nakisi katika urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa kuwa asilimia 7.0 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; na

viii. Kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosheleza mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
Sera za Mapato

56. Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kutekeleza sera zifuatazo:

i. Kuendelea kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato;

ii. Kuendelea kupanua wigo wa walipa kodi ikiwa ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iweze kuingia katika mfumo wa kodi;

iii. Kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na kuboresha usimamizi wake;

iv. Kuendelea kufanya uthamini wa majengo na kusimamia ulipaji ili kuongeza mapato yatokanayo na kodi ya majengo;

v. Kurasimisha miliki za ardhi kwa lengo la kuongeza mapato; na

vi. Kuendelea kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija.

57. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kupanua soko la fedha la ndani ili kuwa na washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi kwenye soko watakaowezesha Serikali kupata fedha za kuziba nakisi kwenye bajeti kwa riba nafuu. Serikali itahakikisha kuwa, mchakato wa upatikanaji wa fedha za mikopo yenye masharti ya kibiashara unaharakishwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa na kuhakikisha fedha zitakazopatikana zinaelekezwa katika miradi ya maendeleo.

58. Mheshimiwa Spika, katika jitihada za Serikali kutaka kuimarisha ushirikiano kati yake na Washirika wa Maendeleo, na kuhakikisha fedha zinazoahidiwa zinatolewa kwa wakati, Serikali na Washirika wa Maendeleo walitafuta Washauri Elekezi Huru. Timu hiyo iliongozwa na Dkt. Donald P. Kaberuka, aliyekuwa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika. Washauri Elekezi walipewa kazi ya kutathmini na kutoa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo na muundo wa utoaji fedha.

59. Mheshimiwa Spika, baadhi ya mapendekezo ya Washauri Elekezi katika kuimarisha ushirikiano yanajumuisha:

i. Kuanzisha Majadiliano Thabiti: Majadiliano hayo yanalenga kufanya mapitio na kuimarisha Mchakato wa Mapitio ya Matumizi ya Umma (PER), kupata matokeo kwenye ngazi ya kisekta pamoja na namna ya kushughulikia masuala nyeti pasipo kuathiri mchakato wa Bajeti.

ii. Kujenga Uwezo wa Kitaasisi: Lengo ni kujenga ujuzi wa kiwango cha juu kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo namna ya kufanya majadiliano ya kuvuna maliasili, masuala ya usimamizi wa fedha, sera za biashara, usimamizi wa deni la nje na utafiti na uchambuzi wa sera.

iii. Kugharamia Azma ya Serikali Kuleta Maendeleo: Hii itahusisha kutafuta fedha kupitia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya Umma. Misaada na Mikopo ya Kibajeti (GBS) bado inaweza kutumiwa katika maeneo mahsusi kama vile kulipia madeni ya Serikali.

60. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kufanyia kazi mapendekezo ya Washauri Elekezi kwa kukamilisha Mwongozo wa Ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo. Mwongozo huu unaainisha masuala mbalimbali ikiwemo: Misingi ya ushirikiano; muundo wa majadiliano; na mifumo ya misaada inayoendana na mahitaji ya nchi. Ni matarajio ya Serikali kwamba, hatua hii itasaidia kuimarisha ushirikiano na hivyo kuwawezesha Washirika wa Maendeleo kutimiza ahadi zao kwa kutoa fedha kwa wakati.
Sera za Matumizi

61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa fedha zinaelekezwa kwenye maeneo ya vipaumbele ili kutekeleza kikamilifu Mpango wa Maendeleo wa Mwaka. Nidhamu ya hali ya juu katika matumizi lazima isimamiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana. Ili kufikia azma hiyo, Serikali itafanya yafuatayo:

i. Kuendelea kuhakikisha kuwa Mashirika ya Umma yaliyoundwa kwa lengo la kujiendesha kibiashara, yanajiendesha kwa faida bila kutegemea ruzuku ya Serikali;

ii. Kuhakikisha mikataba inayoingiwa na Serikali na Taasisi zake inakuwa katika shilingi za Kitanzania isipokuwa kwa mikataba inayohusisha biashara na huduma za kimataifa;

iii. Kuendelea kudhibiti matumizi ya umeme, simu na maji ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia zinazopunguza gharama katika matumizi hayo;

iv. Kuendelea kudhibiti ulipaji wa mishahara kwa kulipa watumishi wanaostahili; na

v. Kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kufanikisha mawasiliano katika shughuli za Serikali.

62. Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti ulimbikizaji wa madeni, Serikali itachukua hatua zifuatazo:

i. Kutokufanya matumizi pasipokuwa na kasma iliyoidhinishwa kwenye bajeti ya Fungu husika;
ii. Kuhakikisha kuwa uagizwaji wa bidhaa unafanyika baada ya kutolewa kwa hati ya ununuzi (LPO) kwenye mfumo rasmi wa malipo (IFMS);

iii. Kuhakikisha kuwa ahadi (Commitment) inafanyika baada ya kupatikana kwa fedha na kutoingia mikataba bila kuwa na ridhaa ya matumizi; na

iv. Kuhakikisha kuwa makubaliano ya kukopa yanafanyika baada ya kupata kibali cha maandishi kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134 pamoja na marekebisho yake.
Maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2017/18

63. Mheshimiwa Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/18 ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21. Kama nilivyoeleza kwenye hotuba ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2016, maeneo ya kipaumbele yanaakisi Mpango wa Miaka Mitano, hususan:

i. Kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda;
ii. Kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu;
iii. Kujenga mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji; na
iv. Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Mpango.

64. Mheshimiwa Spika, Mpango huu umeweka msisitizo katika kufanikisha utekelezaji wa Miradi Mikubwa ya Kielelezo, ambayo ni: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango chaStandard Gauge; Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania; Miradi ya Chuma Liganga na Makaa ya Mawe Mchuchuma – Njombe; Uanzishwaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; Mradi wa Gesi Kimiminika (Liquefied Natural Gas LNG); Kituo cha Biashara cha Kurasini; Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi; na Kusomesha Vijana wa Kitanzania kwa wingi kwenye fani na ujuzi maalum kwa ajili ya maendeleo ya watu na viwanda na kukuza sayansi, teknolojia na ubunifu.

IV. HATUA ZA MAPATO NA MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA NA TOZO MBALIMBALI

A. Hatua za Kisera na Kiutawala
65. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutawala ili kuimarisha na kurahisisha ukusanyaji mapato. Hatua hizo ni pamoja na:

i. Kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kuzuia uvujaji wa mapato ya Serikali. Mfumo uitwao “Government epayment Gateway System” uko tayari kwa ajili ya matumizi ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali. Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali zinaagizwa zianze kutumia mfumo huu;

ii. Serikali imezindua mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (eRCS)) ambao utadhibiti udanganyifu unaofanywa na maafisa wa Serikali kwa kushirikiana na walipa kodi katika kukadiria kodi sahi

0 comments:

Post a Comment