Posted by Williammalecela.com on Friday, August 18, 2017
 |
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kusudio la kufuta leseni ya
Kampuni ya Mycell inayomilikiwa na Quality Group Limited (QGL) ambayo
imekuwa ikiongozwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Yussuf Manji.
Kwa mujibu wa sheria, TCRA iliyoanzishwa mwaka 2003 ina jukumu la
kusimamia, kutoa na kufuta leseni za mawasiliano kwa kampuni yoyote
ambayo imeshindwa kutekeleza majukumu iliyoyabainisha.
“Kampuni ya Mycell imeshindwa kurekebisha ukiukwaji wa masharti ya
leseni”, inasomeka taarifa iliyotolewa na kuwekwa kwenye tovuti ya
mamlaka hiyo.
Kutokana na upungufu huo, “TCRA inauarifu umma kuhusu kusudio la
kufuta leseni za Mycell za kujenga miundombinu kitaifa, kutoa huduma
kupitia miundombinu hiyo, kutoa huduma kupitia mtandao na kutumia masafa
ya mawasiliano”.
Kuonyesha juhudi ilizochukua kabla ya uamuzi huo, TCRA imesema Januari
27, 2016 ilitoa amri ya utekelezaji kwa kampuni hiyo kwa kukiuka
masharti ya leseni walizopewa na kushindwa kutoa huduma kinyume cha
kifungu 21 (a) na (b) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielekrtoniki na
Posta (Epoca) ya mwaka 2010.
Hata hivyo, Mycell haimo kwenye orodha ya kampuni zilizopewa leseni na TCRA ambazo zimo kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.
Mamlaka hiyo imeeleza kwenye taarifa yake ya kusudio la kuifuta Mycell
kuwa iliipa kampuni hiyo leseni nne tofauti Novemba 21,2008.
Inafafanua kuwa leseni hizo ni ya kujenga miundombinu kitaifa, kutoa
huduma kupitia miundombinu hiyo, kutoa huduma kupitia mtandao wa
mawasiliano na kutumia masafa ya mawasiliano.
Kwenye ujumbe wake alioutoa Oktoba, 2011 wakati Quality Group
ikitimiza miaka 35 tangu ianzishwe nchini, mwenyekiti Yusuf Manji
alitanabaisha vipaumbele vya utekelezaji walivyonavyo.
“Mycell inatekeleza mpango wa biashara unaoiruhusu kukodisha masafa
iliyopewa na TCRA kwa kampuni ya nje yenye uwezo na uzoefu mkubwa.
Inatarajia kujenga miundombinu imara itakayofanikisha miradi
mbalimbali”, alisema Manji.
Alisema mpango huo unatokana na fursa kemkem zilizopo kwenye sekta ya
mawasiliano nchini hasa kwa kuzingatia njia za kawaida za kufikishiana
ujumbe ambazo zimekuwa hazikidhi mahitaji yaliyopo kutokana na kukua kwa
kasi kwa teknolojia hasa ya habari na mawasiliano (Tehama).
“Sekta hii ina fursa nyingi kwa kampuni zenye teknolojia ya kisasa
kuwekeza na kukua. QGL inaona kwamba kuna haja ya kuwekeza kwenye
miundombinu na kuziruhusu kampuni za mawasiliano kuongeza ufanisi.
Gharama za kupiga simu na data zipo juu nchini ikilinganishwa na ilivyo
kwa nchi za Asia zinazonufaika na Tehama kwa kiasi kikubwa”, alisema
Manji kwenye ujumbe wake wa mwaka 2011.
Mwaka 1997,Manji alianza kuiongoza QGL akihudumu kama ofisa mtendaji
mkuu kabla ya baadaye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kundi hilo, nafasi
aliyojiuzulu lakini baadaye akarejea tena kuendelea kuiongoza.
Chanzo: MWANANCHI |
0 comments:
Post a Comment