Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta,
amesema ikiwa atashindwa kwa haki, Uchaguzi Mkuu wa tarehe nane mwezi
Agosti, atakubali matokeo na kukabidhi madaraka kwa amani.
Rais Kenyatta ametoa hakikisho hilo
wakati akijibu maswali mbalimbali kupitia runinga na kumtaka mpinzani
wake Raila Odinga, naye kuwa tayari kufanya hivyo ikiwa atashindwa
katika Uchaguzi huo.
Kenyatta amesisitiza kwamba, yeye ni mtu anayeheshimu uamuzi wa wananchi, na kuwaomba wapinzani wake nao wafanye hivyo.
Aidha, amesema serikali yake imelenga
Uchaguzi huo uwe wa amani ndiyo maana maafisa wa usalama wamejihami na
wako tayari kukabiliana na wale watakaotaka kuzua fujo.
Naye Bw. Odinga, anayepeperusha
bendera ya muungano wa upinzani NASA, amekuwa akisema kuwa atakubali
matokeo hayo ikiwa Uchaguzi huo utakuwa huru na haki.
Hata hivyo, hivi karibuni ametoa
madai mazito kuwa Rais Kenyatta anatumia jeshi kumsaidia kuiba kura,
madai ambayo serikali imekanusha.

0 comments:
Post a Comment