Wednesday, March 4, 2015

KLABU ya Azam FC jana Machi 2, 2015 imeachana na kocha wake, Joseph Marius Omog pamoja na kocha Msaidizi namba mbili, Mkenya Ibrahim Shikanda.

Hatua hiyo inafuatia timu kutofikia malengo chini ya Omog hususan baada ya kutolewa katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na El Merreikh ya Sudan mwishoni mwa wiki.

Azam FC ilianza vizuri kwa ushindi wa 2-0 nyumbani Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, lakini ikaenda kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano Khartoum.

Omog alianza kazi Azam FC Desemba 2013 akirithi mikoba ya Muingereza, Stewart John Hall na mwisho wa msimu huo, Mei mwaka jana akaiwezesha timu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, katika msimu wake wa kwanza, Omog alishindwa kufikia rekodi ya Hall katika michuano ya Afrika, baada ya timu kutolewa Raundi ya Awali pia na Ferroviario de Nampula ya Msumbiji Kombe la Shirikisho.

Ikishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika, Kombe la Shirikisho mwaka 2013, Azam FC ilifika Raundi ya Tatu na kutolewa FAR Rabat ya Morocco, baada ya kuzitoa timu za Al Nasr Juba ya Sudan Kusini na Barack Young Controllers ya Liberia.

Hadi anafukuzwa, Omog ameiongoza Azam FC katika mechi 55 za mashindano yote, ikishinda mechi 30, sare 14 na kufungwa 11.
Sasa, Mganda George ‘Best’ Nsimbe anakuwa kaimu Kocha Mkuu wa Azam FC kumalizia msimu wa Ligi Kuu, wakati Bodi ya Ukurugenzi ikiwa katika mchakato wa kusaka kocha mpya.

Jukumu la kwanza la Nsimbe aliyeajiriwa kama Msaidizi wa Omog Januari mwaka huu kutoka KCCA ya kwao, Uganda ni kuhakikisha timu inatetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Hadi sasa, Azam FC inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu kwa pointi zake 27 za mechi 16, ikiwa nyuma ya vinara, Yanga SC wenye pointi 31 za mechi 16 pia.

Nsimbe ataiongoza kwa mara ya kwanza Azam FC Jumamosi itakapomenyana na JKT Ruvu katika Ligi Kuu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.  

Pamoja na kumshukuru Omog kwa kuwaachia taji la ubingwa wa Ligi KuuAzam FC pia inamtakia kila heri katika safari yake Omog.

0 comments:

Post a Comment