Juzi, Rais Jakaya Kikwete aliiagiza Manispaa ya Kinondoni iondoe
maji yaliyozingira nyumba za watu mara moja wakati ikitafakari mipango
ya muda mrefu ya kukabiliana na mafuriko ya maji jijini Dar es Salaam,
ambayo kwa kiasi fulani pia husababishwa na mitaro kujaa uchafu.
Rais Kikwete alitoa agizo kama hili siku chache
wakati alipotembelea eneo la Jangwani na kukuta tatizo kama hilo la
nyumba kuzungukwa na maji na hivyo kusababisha wakazi wengi kushindwa
kuendelea na shughuli zao za kujipatia riziki kutokana na adha hiyo.
Akitoa agizo hilo, Rais alisema kuwa wahandisi
wanajua watawezaje kuondoa maji hiyo kwa kutumia taaluma yao na kwamba
maisha lazima yaendelee na baada ya kuyaondoa ndipo wakae kuangalia ni
jinsi gani watajenga mifereji ili kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.
Tunapenda kumpongeza Rais Kikwete kwa uamuzi huo,
ambao umezingatia kutatua matatizo yanayowakabili wananchi sasa pia
kuangalia baadaye hali hiyo itadhibitiwa vipi.
Huu ni uamuzi ambao wananchi wangependa kuusikia
kwenye matatizo mengine mengi yanayowakumba kila wakati. Mara nyingi
viongozi wa kisiasa hupenda kueleza mikakati mingi mikubwa na ya muda
mrefu wakati kunapotokea tatizo linalohitaji utatuzi wa haraka.
Wakati mvua zilipopamba moto na mafuriko kukumba
sehemu nyingi za Jiji la Dar es Salaam, mamlaka ziliibuka na mpango
mkubwa wa kuliboresha Jiji la Dar es Salaam ambao unahitaji mabilioni ya
fedha kuufanikisha.
Hizi hazikuwa habari ambazo wananchi wangetaka
kuzisikia wakati wakiwa katikati ya matatizo makubwa ya mafuriko, ambayo
yalisababisha barabara nyingi kufungwa na hivyo kusababisha misururu
mikubwa ya magari nyakati zote, hali ambayo kwa kiasi kikubwa iliathiri
utendaji kwenye ofisi nyingi na kuathiri kipato cha wafanyabiashara,
hasa ndogondogo.
Wakati huo, wananchi walitarajia kusikia mamlaka
zimejipangaje kuhakikisha adha wanayopata kutokana na mvua hiyo
inapunguzwa kwa kuchukuliwa kwa uamuzi wa haraka. Wananchi wanajua fika
kuwa mvua kubwa kama hizo hutokea wakati wowote bila ya binadamu kuweza
kuzizuia, lakini wanajua kuwa athari na kero zake zinaweza kupunguzwa
kwa kuwa na viongozi walio tayari kufanya hivyo.
Ndiyo maana Rais Kikwete ameliona hilo na
kuziagiza mamlaka husika kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha maji hayo
yanaelekezwa yanakotakiwa kwenda kwa kuwa mafuriko hayo pia
yamechangiwa na shughuli za binadamu.
Kwa sasa, Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na
tatizo kubwa la foleni za magari na hakuna shaka kwamba tatizo hili
linaathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya mamlaka za jiji na wilaya zake,
kutokana na ofisi nyingi na biashara kutofanya kazi kwa kiwango chake.
Utatuzi wa tatizo hili unaelezewa kwa mikakati
mikubwa ya muda mrefu, wakati hali inazidi kuwa mbaya kadri siku
zinavyokwenda. Hivi wahusika wanataka hadi hiyo miradi ikamilike ndipo
tatizo hili liishe, au wanaweza kuchukua hatua za makusudi kupunguza
tatizo hili?
Tunaamini kwamba kama mamlaka za jiji zitakaa na
kutafakari njia za kupunguza tatizo hili kwa sasa wakati miradi mikubwa
ikishughulikiwa, tatizo hili litapungua na wakazi wataondokana na adha
hii wakati wakisubiri hali nzuri zaidi baadaye.
Uamuzi wa Rais Kikwete kuwataka wahusika Kinondoni na Ilala kutafuta
suluhisho la muda la tatizo la mafuriko, pia uwazindue katika kufikiria
jinsi ya kupata suluhisho la muda la matatizo mengine mengi kama hili la
misururu ya magari.#sourceMwananchi

0 comments:
Post a Comment