Dar/Mashirika. Rais wa Burundi, Pierre
Nkurunziza amewasili jijini Bujumbura ikiwa ni siku mbili baada ya waasi
kutangaza kumuondoa madarakani na tayari majenerali watatu waliotangaza
mapinduzi wamekamatwa huku wanajeshi 12 wakiuawa.
Awali, kulikuwa na taarifa kuwa kiongozi wa uasi
huo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alikuwa amekamatwa pamoja na
wasaidizi wake, lakini baadaye mshauri wa habari wa rais, Willy Nyamwite
alisema alipewa taarifa zisizo sahihi.
Lakini wakati kukiwa na habari kuwa Meja Jenerali
Niyombire amekamatwa, waasi hao wamesema wataendeleza vita dhidi ya
majeshi ya Serikali kwa ajili ya kumuondoa Rais huyo ambaye anapingwa
kutokana na kutangaza kugombea urais kwa mara ya tatu kinyume na katiba.
“Amekamatwa, alikataa kujisalimisha,” Gervais
Abayeho, msemaji wa Rais Nkuruzinza aliliambia Shirika la Habari la
Uingereza, Reuters.
Msafara wa Rais Nkurunziza ulionyeshwa kwenye
televisheni ukiwasili jijini Bujumbura, ingawa picha hizo
hazikumuonyesha Rais huyo ambaye alipitia kijijini kwake Ngozi kabla ya
kwenda jijini humo akitokea Tanzania.
Mnadhimu wa Jeshi, Jenerali Prime Niyongabo,
akizungumza kwa mara ya kwanza tangu majeshi yanayomtii Nkurunziza
yadhibiti redio na televisheni ya serikali, alisema wanajeshi 12 wa
upinzani waliuawa wakati wa mapambano ya kuwania kituo hicho juzi.
Alisema wanajeshi wengine 35 wa uasi walijeruhiwa na 40 wamejisalimisha.
Alisema wanajeshi wanne wa Nkurunziza walijeruhiwa.
Hali ya jijini Bujumbura ilikuwa shwari jana baada
ya mapambano kutawala siku nzima ya juzi wakati majeshi yanayomtii
Nkurunziza yalipokuwa yakipambana kukomboa sehemu muhimu.
“Tunatoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Bujumbura
kufungua tena biashara zao. Hali sasa imesharejea kuwa ya kawaida baada
ya kushindwa kwa waasi,” Meya wa Bujumbura, Saidi Juma aliliambia
shirika la habari la China, Xinhua.
Baada ya kuwasili, Rais Nkurunziza alipewa taarifa
fupi ya mapinduzi na hata jinsi jeshi lilivyofanikiwa kuzima uasi na
kutwaa tena miji ya Bujumbura.
“Rais Pierre Nkurunziza sasa yuko Burundi,” Msemaji wa Serikali, Willy Nyamitwe alisema.
“Hicho ndicho tunachoweza kusema kwa sasa.”
Jenerali Cyrille Ndayirukiye, msaidizi wa kiongozi
wa mapinduzi hayo, alikiri kuwa jitihada za kuuangusha utawala wa
Nkurunziza zimeshindikana.
“Binafsi, nakiri kusema, mipango yetu imekwama,” alisema Jenerali Ndayirukiye.
“Tulipambana tukijua kuwa tutaungwa mkono na jeshi.”
Wakati mapinduzi hayo yakifanyika, Nkurunziza
alikuwa Tanzania kwa ajili ya mkutano wa kutafuta suluhu ya mgogoro wa
Burundi ulioibuka baada ya kiongozi huyo kutangaza kuwa atagombea urais
kwa kipindi kingine cha tatu, kitu ambacho wapinzani wake wanasema ni
kinyume cha katiba.
Mkurugenzi wa kituo kimoja cha redio, Jerome
Nzokirantevye alisema askari wanaomtii Nkurunziza wameshadhibiti sehemu
zote muhimu za Bujumbura, ikiwa ni pamoja na kituo cha redio na
televisheni ya Serikali na Uwanja wa Ndege wa Bujumbura.
Tangu kuanza kwa machafuko hayo, zaidi ya Warundi 100,000 wamekimbilia Tanzania, Rwanda na Uganda.
‘Wanamapinduzi’ wakamatwa
Majenerali wa kijeshi walioendesha jaribio la
mapinduzi, tayari wametiwa mbaroni ikiwa ni saa chache baada ya Rais
Nkurunziza kurejea nyumbani akitumia njia ‘zisizofahamika’.
Hata hivyo, ripoti zilisema kuwa kiongozi wa
mapinduzi hayo, Jenerali Godefroid Niyombare alitoroka muda mfupi baada
ya kuzingirwa na vikosi vya askari wanaomtii Rais Nkurunziza.
Inasadikika kuwa jenerali huyo amejificha kusini mwa mji wa Bujumbura na kwamba wapiganaji wake wanaendelea kushikiliwa.
Maofisa wa jeshi walisema kuwa bado wanaendelea
kumsaka jenerali huyo ambaye awali alikiri kuzidiwa nguvu kiasi cha
kuonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa maisha yake.
Akizungumza na Shirika la Habari la Ufaransa, AFP mapema jana,
Jenerali Niyombare alisema kuwa jaribio la kuiondoa serikali iliyoko
madarakani limeshindwa na wapiganaji wake walianza kujisalimisha.’
Naye msemaji wa waendesha mapinduzi hayo, Venon
Ndabaneze alikiria pia kushindwa kwa jaribio lao akisema kuwa baadhi ya
wapiganaji wao walikamatwa na vikosi vya serikali. Miongoni mwa waasi
wanaoshikiliwa ni pamoja na msaidizi wa kiongozi wa mapinduzi hayo,
Cyrille Ndayirukiye.
Marekani yawaonya raia wake
Marekani imewaonya raia wake kwenda nchini Burundi
na kuwataka wale walioko ndani kuondoka haraka iwezekanavyo. Katika
taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa Burundi
inakabiliwa na hali mbaya ya usalama, hivyo ni muhimu kwa raia hao
kuchukua tahadhari mapema.
Taarifa hiyo iliwataka raia wote wa Marekani
kutotembea ovyo na hata wale wanaotaka kuondoka kuangalia maeneo ambayo
ni salama,” inasema taarifa hiyo.
Hata hivyo, mitaa mbalimbali ya jiji la Bujumbura
ilikuwa imetulia na zaidi walikuwa wakionekana askari wanaomtii Rais
Nkurunziza wakiwa katika vizuizi, ikiwemo Barabara Kuu ya Kusini mwa
Bujumbura.
Uchaguzi Mkuu palepale
Utawala wa Rais Nkurunziza umesisitiza kuendelea na shughuli za Uchaguzi Mkuu ukisema kuwa utafanyika kama ulivyopangwa.
source#Mwananchi
source#Mwananchi

0 comments:
Post a Comment