Uamuzi
wa Rais Dk. John Magufuli, kubana matumizi ya serikali kwa nia ya
kuelekeza nguvu katika kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili
wananchi, umeokoa wastani wa zaidi ya Sh. bilioni 90 katika siku 20
tangu aingie madarakani.
Dk.
Magufuli ambaye aliapishwa Novemba 5, 2015 kufuatia ushindi wake wa
asilimia 58.46 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, ametangaza
maamuzi kadhaa ya kubana matumizi ya serikali ili kuimarisha huduma za
jamii.
Miongoni
mwa maamuzi aliyofanya Rais Magufuli katika siku zake hizo 20 hadi
kufikia jana ni pamoja na kusitisha safari holela za nje, kupiga
marufuku michango ya aina yoyote kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza
hadi kidato cha nne na pia kuamuru kutengenezwa mara moja kwa mashine za
vipimo vya CT-Scan na MRI katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kadhalika,
wiki iliyopita, Rais Magufuli alitangaza pia kufuta sherehe za Uhuru
zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9 na kutaka siku hiyo iadhimishwe kwa
kufanya usafi nchi nzima ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu.
Uchunguzi
uliofanywa na Nipashe kupitia vyanzo mbalimbali umebaini kuwa katika
kipindi hicho kifupi cha siku 20, maamuzi ya Rais Magufuli yameokoa
kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho sasa chaweza kutumika kusaidia
shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kuchimba visima,
kujenga zahanati, kununua magari ya kubebea wagonjwa, kununua madawati
na pia kuweza kujenga viwanja vya soka walau viwili vyenye hadhi kama
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
1. MICHANGO SHULE YA MSINGI
Wakati
akihutubia Bunge kuelezea mapitio ya kazi za wizara yake kwa mwaka wa
fedha 2013/2014, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema wanafunzi
wa darasa la kwanza walioandikishwa mwaka 2014 walikuwa 1,166,497.
Aidha,
uchunguzi wa Nipashe hivi karibuni ulibaini kuwa gharama walizokuwa
wakilipa wazazi kama michango pindi wakipeleka watoto wao kuandikishwa
darasa la kwanza zilikuwa zikitofautiana kati ya shule moja na nyingine,
mfano ni katika Shule ya Msingi Mabatini iliyopo Temeke jijini Dar es
Salaam iliyokuwa ikitoza michango ya jumla ya Sh.25,000, Shule ya Msingi
Kwembe wilaya ya Kinondoni Sh. 67,000 huku shule nyingi za msingi
kadhaa za Wilaya ya Mtwara Vijijini zikiwaandikisha darasa la kwanza kwa
michango yenye thamani ya jumla ya Sh. 9,000. Hivyo, wastani wa
michango hiyo kwa shule walau tatu ni takriban Sh. 35,000.
Ingawa
siyo shule zote za msingi zilizoanza uandikishaji darasa la kwanza
kipindi hiki, bado hesabu zinaonyesha kuwa amri ya Magufuli ya kupiga
marufuku michango ya aina yoyote kwa wanafunzi kuanzia darasa la kwanza
hadi kidato cha nne imesaidia kuwapunguzia wazazi mzigo wa gharama
zitokanazo na michango ya uandikishaji darasa la kwanza.
Kwa
ujumla, kama kila mzazi nchini angeandikisha mwanawe darasa la kwanza
kwa Sh. 35,000, na kama idadi ya wanafunzi hao ni sawa nay a mwaka 2014
ambayo ni 1,166,497, maana yake kiasi cha fedha za michango kwa
wanafunzi wote milioni kingekuwa ni takriban Sh. bilioni 40.83. Amri ya
Magufuli imeokoa fedha hizi kwani sasa wazazi hawatalazimika kuzitoa ili
kaundikisha watoto wao.
2. SHEREHE ZA UHURU
Katika
moja ya makala zilizopo kwenye tovuti yake, Mbunge wa Kibamba, John
Mnyika (Chadema), anasema gharama za sherehe za wiki ya maadhimisho ya
miaka 50 ya Uhuru, Desemba 2011, zilikuwa ni zaidi ya Sh. bilioni 50.
Gharama
hizi zilikuwa kubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa sherehe hizi zilikuwa
na upekee wa aina yake kwani ilikuwa ni nusu karne baada ya uhuru wa
Tanganyika. Hata hivyo, chanzo kimoja kiliiambia Nipashe kuwa gharama za
kawaida za sherehe za siku ya uhuru huwa siyo chini ya bilioni 29. Hizi
huwa ni pamoja na maandalizi kabambe yanayohusisha gwaride la vikosi
vyote vya ulinzi na usalama, ngoma, muziki, halaiki na pia kukaribisha
viongozi wa mataifa mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Kadhalika, jioni
ya siku ya Uhuru huwa na dhifa maalum ya chakula inayoandaliwa na mkuu
wa nchi.
Gharama
nyingine za siku hii ya sherehe za Uhuru huwa ni fedha za kulipa posho
askari wanaoshiriki kwenye gwaride, watumishi wa umma na watoto
wanaoshiriki maonyesho ya halaiki, vinywaji, mafuta ya magari, ndege,
vifaru, vipeperushi, mapambo na gharama nyinginezo.
Kwa
sababu hiyo, uamuzi wa Rais Magufuli kufuta sherehe za mwaka huu za
Uhuru siku ya Desemba 9, 2015 na kutaka siku hiyo isherehekewe kwa kila
mmoja kufanya usafi wa mazingira ili kukabiliana na ugonjwa wa
kipindupindu umeokoa fedha hizo ambazo sasa zinaweza kuelekezwa katika
maeneo mengine ya maendeleo.
3. SAFARI NYINGINE ZA NJE
Katika
hotuba yake wakati akilizindua Bunge Novemba 20, 2015, Dk. Magufuli
alisema anafuta safari zote holela za nje kwa sababu zimekuwa
zikiligharimu taifa mabilioni ya fedha ambayo yangeweza kusaidia
shughuli nyingine za maendeleo kama kujenga barabara za lami za urefu wa
kilomita 400, kuchimba visima vya maji safi na salama na pia kujenga
zahanati au kununua dawa ili kuondoa kero wanayopata wananchi waendapo
kwenye hospitali za umma.
Katika
kutoa mfano, Rais Magufuli alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa
2013/2014 na sehemu ya 2014/2015, taifa lilitumia takriban Sh. bilioni
356. Kwa sababu mwaka mmoja huwa na siku 365, maana yake wastani wa
matumizi ya serikali kwa safari za nje kila uchao ni takriban Sh.
milioni 975.34. Hata hivyo, hesabu hizi ni kwa makadirio kuwa fedha
alizotaja Rais Magufuli zilitumika kwa kipindi cha mwaka mmoja wa
kalenda.
Kwa
sababu hiyo, katika siku 20 za kuwa madarakani kwa Magufuli, yaani
kuanzia Novemba 5, 2015 hadi jana Novemba 25, maana yake kama siyo amri
ya Magufuli, kiasi cha fedha kilichopaswa kutumiwa na taifa kwa ajili ya
safari za nje za vigogo ni takriban Sh. bilioni 19. 51 (yaani siku 20 x
Sh. milioni 975.34). Ukiondoa kiasi kilichohesabiwa katika safari ya
Jumuiya ya Madola, yaani takriban Sh. milioni 700, maana yake fedha
zinazobaki kwa ajili ya safari nyingine za nje zisizokuwa za Jumuiya ya
Madola ni Sh. bilioni 18.81. Wastani wa fedha zote hizo zimeokolewa na
kutokana na amri ya Magufuli hadi kufikia jana na sasa zinaweza kufanya
kazi nyingine za maendeleo.
4. VIPIMO CT-SCAN MUHIMBILI
Kabla
ya kuapishwa kwa Magufuli, vipimo vya CT-Scan katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili vilikuwa vimesimama kufanya kazi kwa zaidi ya miezi miwili
kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ubovu, na pia kuwapo kwa mgogoro
wa malipo baina ya hospitali hiyo na kampuni iliyokuwa zabuni ya kufanya
matengenezo.
Baadhi
ya taarifa zilieleza kuwa kifaa hicho kiliharibika tangu Agosti 30,
2015, hivyo kwa ujumla hadi kufikia jana (Novemba 25, 2015), tayari
zilishatimia siku 85 ziliopita bure bila kifaa hicho kufanya kazi.
Kwa
mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma za Jamii
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaeshi, CT-Scan
inapofanya kazi huhudumia watu 25 hadi 40 kwa siku. Gharama wanazolipia
wagonjwa huwa ni kati ya Sh. 100,000, Sh. 170,000 au Sh. 250,000,
kutegemeana na kundi la malipo la mgonjwa kuwa ni wa ‘private’,
‘general’ au mwenye kadi ya Bima ya Afya.
Kwa
sababu hiyo, ikiwa itachukuliwa kwamba kila mgonjwa huwa wa kujilipia
binafsi (private) na hivyo kulipa Sh.250,000 ili kupata huduma ya
CT-Scan, maana yake gharama zinazokosekana kwa siku kutokana na vifaa
hivyo kutofanya kazi yake huwa ni Sh. 10,000,000; yaani 250,000 x 40.
Jumla ya gharama hizi hadi kufikia jana ambayo ni siku ya 85 tangu
kuharibika kwake ni Sh. milioni 850.
Hata
hivyo, gharama hizo sasa zinaelekea kukomeshwa kwani Rais Magufuli
ameingilia kati kwa kutimua Bodi ya Hospitali hiyo, kumuengua aliyekuwa
akikaimu nafasi ya ukurugenzi na pia kuamuru kutengenzwa vipimo hivyo
mara moja. Mafundi wameshaingia kazini na vilitarajiwa kukamilika jana.
5. HAFLA KUPONGEZA WABUNGE
Hii
ni tafrija maalum iliyokuwa imeandaliwa na Bungeni mkoani Dodoma kwa
nia ya kupongezana kufuatia ushindi walioupata katika uchaguzi mkuu
uliofanyika Oktoba 25, kuapishwa na mwishowe Rais Magufuli kulizindua
Bunge lao la 11, Ijumaa ya Novemba 20, 2015.
Kwa
kawaida, hafla za namna hii ambazo huwakutanisha wabunge wote wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kisha Rais kukaribishwa, huwa na
mbwembwe za kila namna. Waheshimiwa wabunge hula na kunywa watakavyo
huku wakiburudika kwa muziki wa ‘live’ kutoka kwa bendi maarufu za
muziki wa dansi nchini.
Ili
kufanikisha sherehe hizo, yaelezwa kuwa fedha kiasi cha takriban Sh.
milioni 225 kilichangishwa. Hata hivyo, bahati mbaya sana kwa
waheshimiwa wapya wa Bunge la 11, Rais Dk. Magufuli hakukubaliana hata
kidogo na matumzi ya mamilioni yaliyochangwa. Mwishowe, badala ya
kuzimwaga fedha zote hizo kwenye sherehe, akaamuru zitumike kati ya Sh.
milioni 10 na Sh. milioni 15 tu, kisha kiasi chote kilichobaki cha Sh.
milioni 210, kielekezwe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kitumike
kununua vitanda na kuwaondolea wagonjwa adha ya kulala sakafuni.
Kufika
Jumatatu, ikiwa ni siku mbili tu baada ya Magufuli kutoa agizo hilo,
vitanda 300 vilinunuliwa kwa kutumia fedha hizo, pmoja na ziada ya
mashuka 600. Viotu hivyo vyote vimeshafikishwa Muhimbili na wagonjwa
wangali wakinufaika na uamuzi huo wa Rais Magufuli.
6. VIPIMO MRI MUHIMBILI
Kama
ilivyokuwa kwa CT-Scan, mashine ya kipimo cha MRI pia iliharibika kwa
takriban siku 85 hadi kufikia jana. Kwa mujibu wa Eligaeishi, wastani wa
watu wanaopata huduma ya kipimo hiki kwa siku huwa ni 10 hadi 15 na
gharama huanzia Sh. 160,000 kwa wagonjwa wa kundi la jumla (general),
Sh. 350,000 kwa walio na kadi za Bima ya Afya na Sh. 450,000
wanaojilipia binafsi (private).
Ikiwa
wahitaji wote wa huduma ya MRI ni wa kundi la private, yaani
wanaojilipia Sh. 450,000, na ikiwa vipimo hivyo huhudumia idadi ya juu
ya wahitaji ambayo ni watu 15, maana yake serikali ilikuwa ikipoteza
takriban Sh. milioni 6.75 kila uchao au Sh.milioni 573. 75 kwa siku
zote 85 hadi kufikia jana.
Hata
hivyo, mzigo wa gharama zote hizo zinazotokana na ubovu wa kipimo hicho
zinaelekea kukomshwa kwani kutokana na amri ya Magufuli, tayari mafundi
walishaingia kazini tangu wiki iliyopita na kipimo hicho kinatarajiwa
kuanza kazi leo.
7. SAFARI JUMUIYA YA MADOLA
Siku
moja tu baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015, Rais Dk. Magufuli alitoa
maagizo kadhaa yakiwamo ya kuzuia safari holela za nje nchi. Alisema
panapokuwa na ulazima, safari yoyote ni lazima iidhinishwe na yeye (Rais
Magufuli) au Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, lengo likiwa ni kupunguza
matumizi ya serikali ili fedha zinazookolewa zitumike kuboresha huduma
za jamii.
Kutokana
na agizo lake hilo, Rais Magufuli ameripotiwa kufyeka msafara mzito
uliopaswa kuongozwa na yeye mwenyewe na vigogo wengine serikalini
takriban 50 kwenda kwenye mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Madola
unaofanyika barani Ulaya, katika kisiwa cha Malta.
Ikiwa
ni sehemu mojawapo ya kubana matumizi, yaelezwa kuwa ni watu wanne tu
ndiyo walioruhusiwa kwenda kwenye mkutano huo kumuwakilisha Rais
Magufuli na timu yake yote iliyopaswa kuwa kisiwani humo kwa wiki nzima,
ambao ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, balozi mwingine mdogo na
maafisa wengine wawili wa ofisi za ubalozi huo zilizopo jijini London,
Uingereza. Uamuzi huu umeokoa matumizi ya serikali yatokanayo na gharama
za tiketi za ndege na posho za vigogo waliopaswa kusafiri kutoka
takriban Sh. milioni 700 hadi Sh. milioni 49.9 tu.
BILIONI 90.97/- ZAWEZA KUFANYA NINI?
Kwa
ujumla, wastani wa fedha zilizookolewa kutokana na maamuzi mbalimbali
ya Rais Magufuli ndani ya siku 20 za kuwapo kwake madarakani, yaani Sh.
bilioni 90.97, zaweza kufanya mambo mengi ya maendeleo kwa taifa.
Kwa
mfano, akizungumza na Nipashe juzi, Mbunge wa Jimbo la Singida
Magharibi, Elibariki Kingu, alisema wastani wa gharama za kukamilisha
ujenzi wa zahanati hadi kukamilika katika jimbo lake ni Sh. milioni 50.
Kwa
sababu hiyo, kama fedha hizi zikielekezwa katika kujenga zahanati za
kiwango sawa na kile cha Singida Magharibi, maana yake zaweza
kukamilishwa zahanati 1,819.
Wakati
Uwanja wa Taifa ukikamilishwa mwaka 2009, gharama zake zilitajwa kuwa
ni takriban Sh. bilioni 56. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizookolewa
na Magufuli katika siku 20 za kuwa madarakani, yaani Sh. bilioni 90.97
zingeelekezwa kujenga viwanja vya namna ya ule wa Taifa na kutumia
hesabu za wakati huo, maana yake kungekuwa na uwanja mmoja uliokamilika
na mwingine wa pili ungefikia katika hatua muhimu ya kuukamilisha.
Akizungumza
na Nipashe, Kingu (Mbunge wa Singida Magharibi) alisema wastani wa bei
ya bati moja la migongo myembamba mkoani Singida ni Sh. 15,000.
Kadhalika, bei ya mfuko mmoja wa saruji ya ujazo wa Kilogram 50 huuzwa
pia kwa Sh. 15,000. Kwa sababu hiyo, kama fedha hizi zilizookolewa na
Rais Magufuli katika siku 20 za kuwa kwake madarakani zingeelekezwa
kununua vitu hivyo kwa bei kama ya Singida, maana yake ingepatikana
mifuko 6,064,667 ya saruji au mabati ya idadi kama hiyo.
Aidha,
kwa mujibu wa Kingu, gharama ya kuchimba kisima cha maji safi kwenye
jimbo lake huwa ni wastani wa Sh. milioni 15. Hivyo, kama fedha
zilizookolewa kutokana na maamuzi ya Rais Magufuli katika siku 20 za
kuwa kwake madarakani zitaelekezwa kuchimba visima vya kiwango sawa na
vile vya Jimbo la Singioda Magharibi, maana yake vyaweza kupatikana
visima 6,065.
NIPASHE

0 comments:
Post a Comment