Friday, December 25, 2015

 
Mfanyakazi wa Idara ya Maliasili katika Halmashauri ya wilaya ya Lindi, Gasper Msese (49), amefikishwa mahakamani akikabiliwa na shtaka la kumuua kwa makusudi mke wake wa ndoa, Costansia Prince.

Msese alifikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Lindi juzi, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Godfrey Mhini na kusomewa shtaka lake na Mwanasheria wa Serikali, Rehema Mgimba.

Costansia alikuwa ni mtumishi wa Idara ya Elimu akiwa ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlandege, katika Manispaa ya Lindi.

Akisoma hati ya mashtaka, Mgimwa alidai kuwa, Oktoba, mwaka huu, muda wala tarehe isiyofahamika, nyumbani kwao, mtaa wa Kariakoo, mshitakiwa alimpiga mkewe na kusababisha kifo chake.

Alidai baada ya mshtakiwa kumpiga mkewe na kumuumiza, alishindwa kumpa huduma yeyote wala kumpeleka hospitali hadi ndugu wa mke walipofika na kumchukua na kumpeleka Hospitali ya Sokoine ambako alilazwa kwa matibabu.

Alidai kutokana na kitendo hicho, mshitakiwa amefanya kosa kwa mujibu wa kifungu cha 196 ya Sheria ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Hata hivyo mshitakiwa hakutakiwa kukubali wala kukataa kosa, kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi mauaji hadi hapo itakapopelekwa mahakama kuu.

Msese alipelekwa rumande katika gereza lililopo Manispaa ya Lindi na kesi yake PI namba 7/2015, itatajwa tena mahakamani hapo Januari 5, mwakani.

0 comments:

Post a Comment