SERIKALI imekwishatenga
kiasi cha sh. bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya
bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani.
Kauli hiyo imetolewa
jana jioni (Jumapili, Desemba 20, 2015) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa uwanja wa mikutano wa
Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
“Kazi ya utumbuaji
majipu imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugahrimia elimu ya
bure ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa
kampeni. Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza kuisambaza kwa sababu
tunataka shule zikifunguliwa Januari, 2016 watoto waanze kufaidika,”
alisema huku akishangiliwa.
“Atakayezigusa fedha
hizi na kuzitumia vibaya ni lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo
Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Elimu wao na kuwaonya
kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema.
“Hatuhitaji mwanafunzi
achangishwe hela ya mitihani, na zile shilingi 10,000/- kwa ajili ya
wanafunzi wanaosoma Sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa
dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo
tutalazimika kuziombea kibali,” alisema.

0 comments:
Post a Comment