WAHISANI wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP), kwa awamu
ya pili inayoanza utekelezaji wake mwaka huu, wametoa Sh trilioni tatu
ikiwa ni sehemu ya mchango wao katika kuhakikisha kero ya huduma ya maji
kwa wananchi inamalizwa.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alisema hayo jana Dar es
Salaam, wakati akifungua mkutano wa 20 wa wadau wa sekta hiyo na
kuwataja wahisani hao kuwa ni pamoja na Benki ya Dunia (WB), Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Ufaransa.
Lwenge alisema, katika kutekeleza programu hiyo awamu ya pili,
inayotegemea kuanza mwaka wa fedha 2016/17, wahisani hao wametoa Dola za
Marekani bilioni 1.4 (Sh trilioni tatu), na kwamba awamu yote hiyo ya
miaka mitano inagharimu kiasi cha trilioni sita.
“Tumeanza vizuri, wahisani wetu wameahidi kutupa kiasi cha takriban
Sh trilioni tatu, na bajeti ya wizara kwenye programu hiyo ya maji kwa
miaka mitano, tutaiwasilisha bungeni,” Lwenge alisema.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya maji
inaboreshwa na maeneo ambayo haipo inajengwa, pia kulinda vyanzo vya
maji na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma hiyo
muhimu.
Alisema, matarajio ya wizara hiyo ni kumaliza tatizo la maji ifikapo
mwaka 2020, jambo alilosema kuwa linawezekana, kwa sababu kwa sasa
mamlaka za maji na wizara hiyo zinaendelea na kazi ya kuongeza
miundombinu ya maji na kusambaza kwa wananchi.
Alisema, inatarajiwa kuwa hadi ifikapo Machi mwaka huu tatizo la maji
kwa wananchi wa mikoa ya Pwani, ikiwemo Dar es Salaam watakuwa
wameondokana na tatizo hilo, kwa kuwa uzalishaji maji katika mto Ruvu
utakuwa umeongezwa.
Awamu ya kwanza ya Programu ya WSDP, ilianza mwaka 2007 na iliisha
Desemba mwaka jana, kwa miradi mbalimbali ya maji katika mikoa tofauti
nchini kutekelezwa, hali iliyosaidia kupunguza kero ya huduma hiyo.
Awali, akizungumzia ripoti ya maji kwa mwaka jana, Mkurugenzi wa
Programu kutoka Idara ya Uratibu wa wizara hiyo, Dorisia Mulashani
alisema, huduma ya maji vijijini na mijini iliendelea kuboreshwa.
0 comments:
Post a Comment