SERIKALI imeitaja mikoa tisa nchini inayoongoza kwa kuleta watoto
katika Jiji la Dar es Salaam ambao wamekuwa wakiishi mitaani na kuwa
ombaomba ambayo ni Pwani, Iringa, Lindi, Morogoro, Dodoma Mwanza,
Kilimanjaro, Tanga.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangwala
wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha
(Chadema).
Mbunge huyo alitaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuhakikisha
watoto hao wanarudishwa shuleni na kusoma na lini serikali itawachukulia
hatua wale wote wanaotumia watoto hao kuombaomba.
Dk Kigwangala alisema kumekuwa na ongezeko la watoto wanaoishi katika
mazingira magumu na mwaka 2011 Wizara ilifanya utafiti na kubaini
ukubwa wa tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika Mkoa
wa Dar es Salaam ambao ulibaini watoto 5,600.
Alisema baada ya utafiti huo uliandaliwa mradi wa majaribio wa namna
ya kuwaondoa watoto hao mitaani, na kati ya mwaka 2011 hadi 2014, watoto
wapatao 226 waliunganishwa na familia zao, watoto 179 walirudishwa
shuleni.
Pia watoto 196 walipatiwa huduma za afya na 1,000 walipatiwa unasili
na mradi huo ulibainisha mikoa tisa ambayo inaongoza kwa kuleta watoto
jijini Dar es Salaam. Alisema baada ya kufanyika kwa utafiti Wizara
iliandaa mpango kazi unaolenga kuzuia watoto kuingia mitaani,
kuwarejesha na kuwaunganisha na familia zao na kufanya ufuatiliaji.
Alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Septemba 2013 ombaomba 253 na
watoto 135 walirejeshwa makwao kati yao, watoto 33 walirejeshwa shuleni
katika mikoa waliyotoka. Dk Kigwangala alisema zoezi hilo linaendelea
katika mwaka huu wa fedha 2015/2016 ambapo watoto 47 wameunganishwa na
familia zao na kati yao 35 wamerejeshwa shuleni.

0 comments:
Post a Comment